SERIKALI mkoani Rukwa imewaonya waendesha pikipiki maarufu kama boda boda kuacha mara moja kujihusisha kimapenzi na wanafunzi hasa wa shule za msingi na sekondari kwani vitendo hivyo vitawaharibia maisha,kujikuta wakiishia jela na kuziacha familia zao zikiteseka bila msaada wowote.
Mkuu wa mkoa huo Joachim Wangabo alitoa onyo hilo hivi karibuni wakati akikabidhi mkopo wa pikipiki 35 kwa waendesha boda boda ambao ni wanachama wa New bodaboda Saccos iliyopo Manispaa ya Sumbawanga,pikipiki zilizotolewa na Manispaa hiyo ikiwa ni utekelezaji wa kutoa mikopo isiyo na riba kwa makundi maalumu ya vijana,wanawake na watoto katika Manispaa hiyo.
Alisema kuwa baadhi ya waendesha boda boda hao hao wamekuwa na tabia ya kujihusisha kimapenzi na wanafunzi kitendo ambacho ni hatari kwao,nayeye akiwa ni mkuu wa mkoa huo kamwe hatakubali kuona vitendo hivyo ambavyo niwaharibia masomo wanafunzi vikiendelea.
‘’wapo baadhi yenu wamekuwa kikwazo katika kampeni yetu inayoitwa ‘Mwache mtoto asome’ kwani wamekuwa wakijihusisha na wanafunzi kimapenzi,siwezi kuwavumilia……huwa ninawaona mnawabeba wanawake wakubwa,tena warembo kweli wamevaa na mawigi wamependeza si hao wawe wapenzi wenu muwaache wanafunzi wasome?’’……..alihoji mkuu huyo wa mkoa.
Aidha aliwataka pia waendesha pikipiki hao kuzingatia sheria za usalama barabarani pindi wanapo endesha bodaboda hizo kwani wamekuwa wakipuuza sheria hizo kwa makusudi na kusababisha ajali,majeruhi na vifo vinavyoepukika kutokana na uzembe wao.
Wangabo alisema kuwa katika kipindi cha Juni 2019 hadi Juni 2020 mkoa mzima zilitokea ajali 32 za boda boda na jumla ya watu 12 walipoteza maisha kutokana na ajali hizo hivyo kuna haja ya kuendelea kuchukua tahadhari kwa kutii sheria za usalama barabarani ili kupunguza ajali hizo.
Awali akitoa taarifa fupi mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya alisema kuwa halmsahuri hiyo katika mwaka wa fedha 2019/2020 tayari makundi ya walemavu,wanawake na vijana wamekwisha pata mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 235.1
Alisema kuwa mikopo hiyo ambayo ni fedha taslimu na vitendea kazi vimewanufaisha mtu mmoja mmoja wapatao 378 na maisha yao yameanza kubadirika na kuwa bora,huku baadhi yao wakianza kufanikiwa kurejesha mikopo hiyo isiyo na riba.
Mwisho
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.