Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Ndugu Shafi K. Mpenda amelieleza Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo kuwa Halmashauri imefanya manunuzi ya boti mbili za kasi (fiber boat) zenye thamani ya Tsh. 108mil zitakazotumika katika eneo la Uvuvi kwa ajili ya kuimarisha doria katika ziwa Tanganyika kwa maeneo ya Kata ya Kasanga na Samazi.
Ndugu Mpenda ameyasema hayo leo tarehe 29 Julai 2023 katika Mkutano wa Baraza la Madiwani la robo ya nne ambalo ni Baraza la mwisho la mwaka wa fedha 2022-2023, ambapo ameeleza kuwa uundaji wa boti hizo umekamilika na tayari mchakato wa kuziwasilisha unaendelea. Ameongeza kuwa boti hizo zitasaidia kudhibiti uvuvi haramu, ikiwa ni pamoja na kusaidia kudhibiti upotevu wa mapato ya Halmashauri katika eneo la uvuvi pale zitakapowasili.
Aidha Ndugu Mpenda ambaye pia ni Katibu wa Baraza hilo alibainisha kuwa Halmashauri imeanza mchakato wa kuomba kibali cha kutumia kiasi cha fedha zilizobaki katika manunuzi ya boti hizo ili ziweze kutumika kuboresha eneo la Mnada wa Mifugo wa Mkowe, ujenzi wa Machinjio katika Mji wa Matai pamoja na kufanya matengenezo ya boti ya zamani. Hayo aliyasema wakati hakimtoa hofu Diwani wa Kata ya Samazi Mhe. Juma Kibongwe baada ya kuonesha wasiwasi wa kutelekezwa kwa boti ya zamani ambayo inaweza kufanyiwa matengenezo na kuendelea kutumika. Halmashauri ilipokea kiasi cha Tsh. 300mil kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ajili ya ununuzi wa boti ili kuimarisha eneo la Uvuvi.
Katika Baraza hilo hoja mbalimbali ziliwasilishwa na kujibiwa, hoja hizo zilielekezwa katika maeneo mbalimbali ya kisekta na kiutendaji ikiwa ni pamoja na;
Ukusanyaji Mapato;
Mkurugenzi Mtendaji Ndugu Shafi M. Mpenda amelieleza Baraza wa Madiwani kuwa Halmashauri ina jumla ya mashine za kukusanyia mapato (POS) 126 ikiwa ni ongezeko baada ya kufanya manunuzi ya Mashine mpya za Kukusanyia mapato (POS) 85 ambazo tayari zimewasili na utaratibu wa kuzipeleka katika maeneo ya ukusanyaji katika Vijiji vyote 111 vya Halmashauri unaendelea. Aidha Ndugu Mpenda ametumia nafasi hiyo kuwataka Waheshimiwa madiwani kuhakikisha kila Shilingi ya mapato inakusanywa kupitia mashine hizo katika maeneo yao. Hayo yalisemwa ikiwa ni majibu kwa Diwani Kata ya Kilesha Mhe. Paul Luwis aliyehoji juu ya Halmashauri kupoteza mapato katika maeneo mbalimbali kutokana na uhaba wa mashine za kukusanyia mapato. Upungufu huo ulitokea kufuatia mabadiriko ya mfumo wa kukusanyia mapato ambapo mfumo mpya wa TAUSI unahitaji mashine zenye uwezo zaidi ya zile zilizokuwa zikitumika katika mfumo wa awali.
Elimu;
Akitoa ufafanuzi juu ya Mwongozo wa kitaifa wa utoaji wa huduma ya chakula na lishe kwa wanafunzi elimi msingi Afisa Elimu Secondari Ndug. Ramadhan Mabula amelieleza Baraza kuwa ofisi za Kata kupitia Baraza lake zinawajibu wa kusimamia upatikanaji wa chakula katika shule za Msingi zilizopo katika maeneo yake ikiwezekana kwa kupeana adhabu ili kutimiza lengo lililokusudiwa. Hayo yalisemwa ikiwa ni majibu ya swali la Diwani Kata ya Lyowa Mhe. Benard Mwamsojo alipotaka kujua Serikali na Halmashauri zinampango gani kuweka sheria itakayowabana wazazi wanaoshindwa kuchangia chakula shuleni ili kufanikisha mpango huo kutokana na wazazi wengi kutochangia mpango huo.
Maendeleo ya Jamii;
Afisa Mipango Takwimu na Ufuatiliaji Ndugu Erasto Mwasanga amelieleza Baraza la Madiwani kuwa Halmashauri imepokea hoja ya changamoto ya fedha za mpango wa TASAF kutowafikia walengwa ambapo changamoto hiyo itafanyiwa kazi kuona namna ya kuboresha zaidi. Akiwasilisha changamoto ya walengwa kutonufaika na fedha za mpango kutokana na njia ya mitandao ya simu inayotumika kupokelea fedha, Diwani wa Viti Maalum Mhe. Constansia Nyembele amesema baadhi ya wanufaika wanakumbana na changamoto hiyo kutokana na watu wao wa karibu wasiowaaminifu kutoa fedha na kuzitumia bila kufikisha kwa mlengwa, hii ni kutokana na wanufaika wengi kutumia namba za simu za watu wao wa karibu kupokelea fedha.
Aidha katika eneo hilo Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Daud Nzelani amewakumbusha Waheshimiwa madiwani kuwa wana jukumu la kupitia na kufanya marekebisho ya miradi ya barabara na vivuko inayoibuliwa na wananchi katika maeneo yao pale inapobidi, ili kuepusha malalamiko baada ya utekelezaji kuanza kufanywa na mradi wa TASAF.
Kilimo;
Diwani wa kata ya Matai Mhe. Vitus Tenganamba aliwasilisha changamoto ya uharibifu wa mazao ya kilimo unaofanywa na Tembo katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri huku akitaka kujua ni lini Serikali itatoa fidia kwa wahanga wa uharibifu huo. Akiongezea changamoto hiyo Diwani wa Kata ya Kasanga Mhe. Leopard Mbita ameeleza uwepo wa Boko wanaofanya uharibifu katika mwambao wa ziwa Tanganyika kwa maeneo ya Kasanga na Samazi. Akijibu kuhusu fidia Afisa Maliasili na Mazingira wa Halmashauri Ndugu Magreth Kakoyo amewataka wananchi kuendelea kusubiri kwa kuwa suala ya fidia ni mchakato ambapo kama Halmashauri imewasilisha tathimini ya uhalibifu uliofanywa na tembo kwa Wizara husika ambayo ndio yenye jukumu ya kulipa fidia. Kuhusu changamoto ya wanyama Boko amelieleza Baraza ya Madiwani kuwa Halmashauri itafanya mawasiliano na ngazi za juu ili kuona uwezekano wa uwahamisha wanyama hao.
Utawala;
Aidha katika Baraza hilo wajumbe waliibua tena suala la mgogoro wa mpaka uliopo kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo na Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga kwa kutaka kuondoshwa kwa kibao kinachotenganisha maeneo ya Mamlaka hizo mbili kilichowekwa kimakosa, ata hivyo Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Rukwa Ndugu. Mfaume Mpapalika Mfaume aliwasihi Waheshimiwa Madiwani kuwa na Subra kwa kuwa tume ya kuchunguza mgogoro huo ilishawasilisha ripoti katika ofisi ya Katibu Tawala ambapo muda wowote ripoti hiyo itawekwa wazi.
Katika kuhitimisha Mkutano wa Baraza hilo Waheshimiwa Madiwani wametakiwa kuwaeleza wananchi wa Halmashauri wa Wilaya ya Kalambo kuacha kuchoma moto hovyo maeneo ya kilimo kwani uchomaji huo umekuwa ukihatarisha uoto wa asili pamoja na miundombinu mbalimbali ikiwemo nguzo za Umeme.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.