Mkuu wa wilaya ya Kalambo Julieth Binyura amewataka wananchi wa kijiji cha Kipwa kilichopo mpakani mwa nchi ya Tanzania na Zambia mwambao wa ziwa Tanganyika kuhamia katika maeneo ya miinuko kwa lengo la kuondokana na adha ya kujirudia kwa matukio ya nyumba zao kuzama kwa maji.
Hatua hiyo inakuja baada ya Zaidi ya nyumba 79 kubomoka na kaya themanini kukosa makazi kutokana na nyumba zao kubomoka kufuatia maji ya ziwa Tanganyika kuzingira makazi yao na kupelekea baadhi yao kukosa makazi.
Akiwa ofisini kwake mkuu wa wilaya hiyo Julieth Binyura amesema wananchi hao wanapaswa kuhama maeneo hayo kutokana na kuwa hatarishi kwa maisha yao na kuwasihi kuhamia katika maeneo ya milima iliyopo karibu na kijiji chao ambako maji ya ziwa hilo hayawezi kufika kwa urahisi kuliko hivi sasa.
Awali wakizungumzia mkasa huo viongozi wa serikali ya kijiji hicho, walisema tukio kama hilo ni la pili kujitokeza, ambapo kwa mara ya kwanza liliwahi kutokea mwaka 1984.
“tuna kila sababu ya kuhamia maeneo ya milimani na kuanzisha makazi ya kudumu, kwani mpaka hivi sasa wananchi wetu hawana makazi tena kutokana na nyumba zao kubomoka kutokana na maji ya ziwa Tanganyika kuhamia kijijini” alisema Divan Mwimanzi kaimu mwenyekiti wa kijiji hicho.
Mtendaji wa kijiji hicho Leo Samsoni Katonto , alisema watu wote waliokubwa na kadhia hiyo wamehifadhiwa kwenye majengo ya taasisi za dini na serikali wakati wakisubiri maji kupungua.
“nyumba 80 zimebomoka na kaya 80 zimekosa makazi na nyumba 60 ziko hatiani kuanguka na watu wote waliopatwa na adha ya kubomokewa nyumba zao tumewahifadhi kwenye majengo ya taasisi za serikali na za dini” alisema Katonto.
Afisa tarafa ya Kasanga Edrue Ngindo, alikiri kutokea adha hiyo na kusema wamewaelekeza wananchi kuhamia katika maeneo ya miinuko ili kuepukana na adha hiyo na kusema watu wengi wamekosa makazi kutokana na maji ya ziwa hilo kuzingira maeneo ya makazi yao.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.