Halmashauri ya wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa imepokea fedha jumla ya shilingi milioni 529.6 ambazo zitasaidia kuondoa mlundikano wa wanafunzi katika shule 14 za msingi na sekondari pamoja na kujenga matundu ya vyoo katika shule hizo huku mkuu wa mkoa huo Joachim Wangabo akitoa miezi miwili kwa uongozi wa halmashauri hiyo kuhakikisha ujenzi huo unakamilika.
Wangabo ameyasema hayo alipotembelea miradi ya Lipa kulingana na Matokeo (EP4R) na Miradi ya Afya na Usafi wa Mazingira (SWASH) inayotekeleza ujenzi wa madarasa na vyoo vya wananfunzi kwa shule za msingi na Sekondari Wilayani Kalambo ambapo wilaya hiyo imepokea jumla ya Shilingi 529,679,504 kwa mwaka huu wa fedha ili kutekeleza miradi hiyo.
Awali wakati akisoma taarifa ya miradi hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, Afisa Mipango wa Halmashauri hiyo Eric Kayombo alisema kuwa Shilingi 353,900,000 ilipokelewa katika shule saba za msingi kwaajili ya ujenzi wa madarasa na vyoo na Shilingi 175,776,504 ilipokelewa katika shule nyingine 7 za msingi kwaajili ya ujenzi wa vyoo.
“Mheshimiwa Mkuu wa mkoa utekelezaji wa miradi hii umeanza mwaka huu wa fedha 2020/2021 badala ya mwaka 2019/2020 hii ni kutokana na Halmashauri kupokea fedha za miradi mwishoni mwa mwaka wa fedha 2019/2020 na kufanya kuvuka mwaka na kuanza kutekeleza mwaka huu wa fedha, Miradi ya EP4R ipo katika hatua za msingi na miradi ya afya na usafi wa mazingira ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji,” Alisema.
Mh. Wangabo ametoa miezi miwili kwa halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kuhakikisha wanamaliza miradi hiyo kwa shule za msingi na sekondari ili kuimarisha miundombinu ya shule hizo ambazo Miradi hiyo inatekelezwa ikiwemo shule ya sekondari ya Wasichana Matai ambayo inatarajiwa kuanza kupokea wananfunzi kuanzia mwaka 2021.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.