Mkuu mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo ameitaka mamlaka ya maji safi Sumbawanga SUWASA kumaliza changamoto ya maji katika miji midogo ya halmashauri zote za mkoa huo kwa kukaa na Wataalamu wa Wizara husika na kuandaa utaratibu ambao utasaidia wananchi kuondokana na adha ya ukosefu wa huduma ya maji.
Ameyasema hayo alipotembelea mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji safi unaoendelea kujengwa katika mji mdogo wa Namanyere ili kujionea maendeleo ya mradi huo pamoja na kujua changamoto zinazoukabili na hatimae kuona namna ya kuupatia ufumbuzi huku akiwa ameambata na kamati ya ulinzi na Usalama ya mkoa pamoja na wataalamu wengine kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa.
Amesema kuwa awali wananchi waliaminishwa kuwa baada ya upanuzi wa bwawa la mfili shida ya maji ingekuwa imekwisha, lakini matokeo yake baada ya upanuzi huo bado shida ya maji imeendelea kuwepo ambapo sasa kuna mradi wa ujenzi wa matenki mapya ambayo hayatakidhi mahitaji ya maji katika mji huo unaokuwa kwa kasi na hivyo kuwataka kujipanga kumaliza tatizo hilo.
“Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi inasema huku kwenye miji mikuu ya wilaya inatakiwa kupata maji kwa asilimia 85, ninyi mtatoa asilimia 46, sasa SUWASA mkae na Wataalamu wa Wizara husika ya Maji muandae utaratibu ukae tayari tayari juu ya namna gani ya kuweza kukimbiza huu mradi, watu wamechoshwa na subiri subiri hata waswahili wanasema ngoja ngoja yaumiza matumbo,” Alisisitiza.
Awali akisoma taarifa ya mradi huo meneja wa SUWASA Mhandisi Gibon Nzowa alisema kuwa shida inayosababisha mradi huo kutofikia asilimia 85 ya upatikanaji wa maji katika mji huo ni kutokana na kutokuwepo kwa mtandao wa kuyasambaza maji hayo kwa kilomita 15 lakini maji yalipo katika chanzo yanatosheleza kwa asilimia 85 endapo tatizo la mtandao litatuliwa na kisha kueleza shughuli za mradi huo.
“Kazi zinazotekelezwa ni ununuzi na ufungaji wa pampu mbili za kusukumia maji, ulazaji wa bomba kuu kutoka bwawa la mfili hadi kwenye tenki takriban kilomita 3.7, pia ujenzi wa tenki la lita 500,000 ambalo limeinuliwa kwa mita 12 ili kuwezesha maeneo mengi ya Namanyere kupata maji, ulazaji wa mtandao wa usambazaji maji kwa kilomita 6.5, vile vile katika mradi huu kutakuwa na dira za maji za kuunganishia wateja,” Alimalizia
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda wakati akielezea hatua walizochukua kupambana kumaliza tatizo hilo la upatikanaji wa maji katika mji wa Namanyere alisema kuwa kama wilaya walikaa na kuandika andiko na kuhitaji Shilingi Bilioni 2.5 na kuliwasilisha wizarani ambapo fedha hiyo ilipunguzwa hadi kufikia shilingi Bilioni 1.5 hali iliyopunguza asilimia ya upatikanaji wa maji katika mji huo.
“Tulitafuta wataalamu wakaandika huu mradi, wakaleta kwangu tukapitia tukaona ni mradi wa Shilingi bilioni 2.5 ambayo hiyo ingetuwezesha kusambaza maji maeneo yote yenye upungufu wa maji katika mji wetu, kwahiyo Waziri alipokuja tulimkabidhi akasema tuwape SUWASA nao baada ya kuipiti walipeleka wizarani ambapo wakapunguza kiwango cha fedha, huu mradi ulikuwa ni wa Bilioni 1.8 lakini Mheshimiwa waziri akasema ipungue hadi kufikia shilingi bilioni 1.5 lakini kama ingekuwa ule mradi wetu wa Shilingi bilioni 2.5 tungekuwa na mtandao wa kilomita 15 kuliko huu wa sasa wa kilomita 6,” alisema.
Mradi huo wa uboreshaji wa huduma ya maji safi katika mji wa Namanyere unatarajiwa kumalizika mwezi Mei mwaka 2020 na kugharimu shilingi Bilioni 1.58 fedha zinazotolewa na serikali huku ukitarajiwa kuhifadhi maji kutoka lita 350,000 hadi lita 850,000 na kufikia asilimia 46 ya uaptikanaji wa maji katika mji huo.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.