JAJI Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma ameutaka uongozi wa mkoa wa Rukwa kuto tegemea sheria pekee kama mwarobaini wa kumaliza tatizo la mimba za utotoni badala yake jamii nzima ihusishwe katika kutafuta suluhu ya changamoto hiyo.
Aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na viongozi wa mkoa wa Rukwa wakati wa ziara yake ya siku mbili ya kutembelea na kukagua utendaji wa mahakama katika wilaya zote tatu za mkoa huo.
Alisema suala mimba za utotoni inabidi kuishirikisha jamii moja kwa moja ili kuzungumza kwa lugha moja na kuja na suluhu ya changamoto hiyo na si kutegemea sheria pekee ndio zitamaliza tatizo hilo.
Hata hivyo, mkuu wa mkoa huo Joachimu Wangabo alisema katika kikao hicho kuwa katika mwaka huu mkoa una mimba za utotoni 294, ambapo tayari kuna mpango mikakati umeandaliwa utakaoshirikisha wadau wote katika kudhibiti changamoto hiyo.
Alisema hivi karibuni kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) kitaketi moja ya ajenda itakuwa ni kujadili mikakati ya namna ya kukabiliana na tatizo hilo sugu mkoani humo, na utekelezaji wake utaanza mara moja.
Katika hatua nyingine jaji mkuu wa Tanzania alisema kuwa mahakama inaangalia uwezekano wa kuanza utaratibu wa kutoa nakala za hukumu kwa lugha ya kiswahili ili kuwarahisishia wananchi upatikanaji wa haki katika vyombo vyake vya maamuzi.
Alisema kuwa hoja ya mahakama kutoa nakala za hukumu kwa lugha ya kiswahili ni jambo la msingi na litasaidia upatikanaji wa haki kwa wananchi wanaofika mahakamani kutafuta haki juu ya mashauri mbalimbali.
Alisema pia itawasaidia kufahamu na kuelewa kwa urahisi kile kilichoamuliwa na mahakama, hivyo yule anayetaka kukata rufaa mahakama ya juu inakuwa rahisi kwake kufanya hivyo na kwa wakati sahihi.
"Hii hoja ya kutumia lugha ya kiswahili katika mahakama zetu ni jambo la msingi na muhimu sana.....tumeipokea na tutaifanyia kazi" alisema
Hoja hiyo, iliibuliwa na mkuu wa wilaya ya Sumbawanga, Dk. Halfan Haule ambaye alidai wanaiomba Mahakama kuona umuhimu wa kutoa nakala za hukumu kwa lugha ya kiswahili ili wananchi wawe na uelewa wa kile kilichoamuliwa kuliko ilivyo sasa ambapo wengi wao hutembea na nakala ya hukumu kutafuta wakalimani hadi inachakaa.
Alisema kuwa hata wale wanaohitaji kukata rufaa baada ya kutoridhishwa na hukumu ya awali hujikuta wakichelewa kufanya hivyo kutokana kutumia muda mwingi kutafuta wakalimani ambao wakati mwingine wanahitaji fedha.
Dk. Haule alisema hali hiyo imesababisha wananchi wengi kupoteza haki zao za msingi kutokana na kuto elewa kile kilichoandika katika hukumu iliyotolewa na mahakama husika kwani angefahamu mapema labda angeweza kukata rufaa.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.