Halmashauri ya wilaya ya Kalambo imefanikiwa kuingiza zaidi ya asilimia 80 ya taarifa za fedha za shule za msingi, Sekondari, Zahanati pamoja na vituo vya Afya katika mfumo wa FFARS. Mafanikio hayo yamefikiwa kufuatia mafunzo ya siku 3 kwa Wakuu wa shule za msingi na sekondari, Wasimamizi wa zahanati pamoja na wasimamizi wa vituo vya afya. Mafunzo hayo yalifanyika kwa jumla ya siku 9 huku kukiwa na makundi matatu ya washiriki ambapo kila kundi lilipata mafunzo hayo kwa muda wa siku 3. Jumla ya washiriki 158 kutoka shule za msingi 98, shule za sekondari 15 na vituo vya afya 45 walishiriki katika mafunzo hayo yaliyoenda sambamba na uingizaji wa taarifa za fedha za vituo hivyo kuanzia mwezi Julai 01 hadi sasa. Wataalam kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo kwa kushirikiana na Wataalamu kutoka mradi wa PS3 kwa pamoja walifanikiwa kuendesha mafunzo hayo yaliyoleta tija kubwa kwa vituo hivyo vya kutolea huduma na Halmashauri kwa Ujumla.
Changamoto mbalimbali zilijitokeza Katika zoezi hilo ambapo baadhi ya washiriki kutoka katika vituo 13 walishindwa kuhudhuria mafunzo hayo kutokana na sababu mbalimbali. Changamoto nyingine ni uhaba wa vitendea kazi (kompyuta) kwa ajili ya uingizaji wa taarifa ambapo kompyuta moja ilikuwa ikitumiwa na washiriki watano hadi sita jambo ambalo lilipelekea zoezi hilo kutokwenda kwa wakati, huku changamoto kubwa ni vituo vingi vya kutolea huduma kutokuwa na kompyuta ambazo zingeweza kutumika katika uingizaji taarifa fedha katika mfumo wa FFARS na shughuli nyingine pamoja na ukosefu wa huduma ya intaneti ya uhakika katika maeneo ya vituo vya kutolea huduma. Aidha changamoto ndogo ndogo zimebainika katika mfumo wa FFARS ambapo zitawasilishwa OR-TAMISEMI kwa ajili ya maboresho na kuufanya mfumo huo kuwa bora zaidi.
Mafunzo hayo yalifunguliwa na Afisa Elimu Sekondari Bw. Ephraim Moses kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo katika ukumbi wa Sun rise, Matai tarehe 12 Februari ambapo washiriki waliaswa kuzingatia mafunzo hayo ikiwa ni pamoja kuzingatia miongozo mbalimbali ya matumizi ya fedha za Umma katika vituo vyao vya kutolea huduma ili fedha hizo zitumike kwa shughuli zilizokusudiwa. Aidha Mafunzo hayo yaliitimishwa na Kaimu Mganga Mkuu Wilaya ya Kalambo Dr. Tusekile Kasanga tarehe 21 Februari na kuwataka wasimamizi wa vituo kuwa jirani zaidi na Jamii ili kufanikisha zoezi ya utoaji wa Huduma za afya. Uingizaji wa taarifa hizo unatarajiwa kufikia asilimia 100 ifikapo tarehe 28 ya mwezi wa Februari Mwaka huu kufuatia uingizaji unaoendelea kufanywa na vituo hivyo vya kutolea huduma. Mfumo huo wa FFARS unatarajiwa kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utendaji wa kazi ikiwa ni sambamba na upatikanaji wa taarifa za fedha za Vituo vya kutolea huduma kwa wakati.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.