Halmashauri ya wilaya ya kalambo mkoani Rukwa kupitia idara ya mifugo na uvuvi imenza kukabiliana na wimbi la mbwa vichaa kwa kuwapiga risasi baada ya kujitokeza malalamiko ya wananchi katika maeneo tofauti ya wilaya hiyo wakidai kung’atwa na kusababishiwa madhara mbali mbali yakiwemo tetenasi,kichaa cha mbwa na hatimaye kupoteza maisha.
Hatua hiyo inakuja baada ya mbwa mmoja aliyesadikiwa kuwa na kichaa kung’ata watoto kumi na nne katika vijiji vya Keleni na Matai asilia, watu wazima watatu Kisungamile na mtu mzima mmoja katika kijiji cha Santa Maria ambaye pia alipoteza maisha. Kufuatia matukio hayo, wananchi wamelazimika kuiomba serikali kuangalia namna ya kuwasaidia kwa kuawapatia chanjo mbwa wote.
‘’Tunaiomba serikali iangalie uwezekano wa kuwa chanja mbwa wote pamoja na kusogeza huduma ya chanjo ya kuzuia kichaa cha mbwa kwenye Vituo vya Afya na Zahanati zote, badala ya kufuata huduma hiyo mjini Sumbawanga baada ya kung’atwa na mbwa ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakichelewa na hatimaye kupoteza maisha.’’Walisema wananchi hao.
Akiongea kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Santa Maria, Afisa mifugo na uvuvi wilayani humo Wilbroad Kansapa, amesema wilaya hiyo inajumla ya mbwa wapatao 6,360 na kwamba ili kukabiliana na changamoto hiyo amewasiliana na Mganga Mkuu wa wilaya ili kuhakikisha dawa za kuwatibu watu ambao wamekuwa wakiathirika na adha hiyo zinapatikana kwenye vituo vyote vya afya na zahanati katika Wilaya nzima.
Wakati huo huo ,amewataka wananchi wote wanaomiliki mbwa kuwaleta mbwa wote kuchanjwa pindi tangazo linapotolewa, na kwamba mbwa wote lazima wafungwe kuanzia saa kumi na moja asubuhi na kufunguliwa saa sita usiku, vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao wote watakao kaidi sheria hiyo, lengo likiwa ni kuendeleza azima ya Serikali ya kufuga kitaalamu na kwa tija nchini kote.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.