Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule amepokea maghala matatu yenye thamani ya shilingi 322,989,901/= Yenye uwezo wa kuhifadhi tani 1980 yaliyojengwa na shirika la MIICO kwa udhamini wa Kampuni ya Agra Africa.
Maghala hayo yaliyojengwa katika vijiji vya Sakalilo, Wilayani Sumbawanga, Katete Wilayani Kalambo na Katongolo Wilayani Nkasi yanalenga kuwanufaisha wakulima wa vijiji hivyo kuimarisha uhifadhi wa mazao yao ambapo wakulima wengi katika mkoa wamekuwa wakiuza mazao yakiwa shambani au mara baada ya kuvuna kutokana na kukosa sehemu za kuyahifadhi.
Wakati akitoa shukrani zake Dkt. Haule alisema kuwa wakulima wengi katika Mkoa wa Rukwa wamekuwa wakiuza mazao yao mara baada ya kuvuna ili kukidhi mahitaji mbalimbali yanayowakabili na kiasi kinachobakia kimekuwa kikihifadhiwa katika nyumba zao. Hifadhi hizi si salama na ni hatarishi pale wanapotumia viuatilifu kwa ajili ya kuua na kuzuia wadudu waharibifu.
“Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imekuwa ikiweka mikakati ya muda mrefu na mfupi ya kutatua changamoto za uhifadhi wa mazao katika Mkoa. Mikakati hiyo ni pamoja na kukarabati maghala yaliyopo katika Mkoa na kujenga maghala mengine.Katika mkakati wa ujenzi wa maghala nashukuru shirika la MIICO kwa kujenga maghala Matatu katika Mkoa wetu,” Alisema.
Aidha ameongeza kuwa, Serikali kupitia NFRA inajenga vihenge vya kisasa vya kuhifadhia mahindi katika eneo la Kanondo. Baada ya kukamilika kwa ujenzi huo NFRA watakuwa wameongeza uwezo wa kuhifadhi mahindi kwa tani 25,000 na kufanya uwezo wao wa kuhifadhi nafaka kufikia tani 58,500.
Kwa upande wake Meneja wa Agra Mkoa wa Rukwa na Katavi Japhet Laizer aliiomba serikali kuona namna ya kuweza kuvisaidia vyama vya ushirika kwa kuwaondoa viongozi wabovu katika vyama hivyo ambao wanarudisha nyuma maendeleo ya wakulima wengi na kusababisha wakulima kutokuwa na Imani na vyama hivyo na hivyo lengo la serikali la kuunganisha wakulima kushindwa kufanikiwa kama inavyotarajiwa.
“Tunaiomba serikali, wawe mara kwa mara wanajitahidi kuvipitia hivi vyama vya ushirika, vya ma vya ushirika kwa upande mwengine vimekuwa ndio vya kupiga na kuwaumiza wakulima, hivyo tunaiomba serikali ipitie mara kwa mara katika kutatua changamoto za vyama vya ushirika ili mwisho wa siku tuone wakulima wananufaika na uwekezaji huu, katika taarifa mmeweza kusikia pia tumewekeza katika sekta binafsi, ukipitia kwenye maghala yanayosimamiwa na watu binafsi unakuta mazao yamejaa mpaka hakuna nafasi, lakini ukienda kwenye maghala yanayosimamiwa na vyama vya ushirika unakuta hakuna hata gunia moja la mahindi,” Alisisitiza.
Mkoa una maghala 82 yenye uwezo wa kuhifadhi jumla ya tani 56,300 tu. Uwezo huu wa kuhifadhi ni sawa na asilimia 19.15 tu ya ziada ya mahindi tunayozalisha katika Mkoa.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.