Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya amepata fursa ya kutembelea soko kuu la samaki Kasanga Wilayani Kalambo ambalo linategemewa kukusanya zaidi ya shilingi million mia moja kwa mwaka.
Katika ziara yake, alikutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo ambapo kwa pamoja walikubaliana kuweka nguvu katika kuendeleza soko hilo ikiwemo kulitangaza kwa lengo la kuvutia wafanya biashara wa ndani na nje ya nchi.
Soko hilo ni moja kati ya masoko mawili ya kimataifa yaliyopo Wilayani Kalambo ambapo soko linguine ni la mazao lililopo katika mji wa Matai, yaliyojengwa kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2011 kupitia mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA] kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kabla haijamegwa na kuzaliwa Wilaya mpya ya Kalambo, huku ujenzi wake ukifadhiliwa kwa asilimia 80 na jumuia ya Ulaya (EU).
Lengo la mradi huo, ilikuwa ni kuwaunganisha wakulima ili wawe na sauti moja katika kushawishi na kutetea maslahi yao kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kisiasa.
Soko la kimataifa la kuuzia samaki liko umbali wa kilomita 73 kutoka mji wa Matai ambao ndio makao makuu ya Wilaya likilenga kuwanufaisha watu 35,205 wa ukanda wa ziwa Tanganyika na watu 238,000 kutoka maeneo mengine ya Wilaya ya Kalambo, sumbawanga na mikoa jirani ya Mbeya,Iringa, Njombe na Ruvuma pamoja na nchi jirani za Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda na Burundi ambapo mapema tarehe saba Machi mwaka huu, soko hilo lilizinduliwa rasmi na kuanza kufanya kazi iliyokusudiwa.
Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo,imewataka wafanyabiashara wote wa samaki wa ndani na nje ya nchi kufika kwa wingi katika soko hilo ili wapate samaki kwa wingi na wenye ubora wa kiwango cha kimataifa kwa ajili ya kukuza mitaji yao kwa maendeleo ya Kalambo na taifa kwa ujumla.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.