NAIBU Waziri wa afya na ustawi wa jamii Godwin Mollel amekiri kuwepo kwa changamoto juu ya mfumo wa bima ya afya ya jamii na kuwa wizara imeliona na inakwenda kulifanyia kazi.
Hilo amelisema jana alipokuwa akizungumza na Watumishi wa idara ya afya wa wilaya Nkasi kwenye jengo jipya la hospitali ya wilaya baada ya kupata malalamiko kutoka kwa mbunge wa jimbo la Nkasi Kasikazini Aida Khenan ambaye alisema kuwa huduma za afya kupitia bima hazina uhalisia wa kile kinachotarajiwa.
Alisema kuwa kinachoangaliwa sasa ni mfumo wenyewe wa bima ambapo kwa sasa fedha zinaenda ofisi ya mkuu wa mkoa na baada ya hapo kuna asilimia zinazokwenda wilayani hadi vituo vya afya na kuwa hilo wameliona na watakwenda kutafuta ufumbuzi wa hilo ili kasoro zitakazobainika ziondolewe.
Pia Mollel aliitumia fursa hiyo kuwafunda watumishi wa afya kufanya kazi zao kwa weredi na kuwa wao kama wizara wamebaini mambo mengi ya hovyo yanayofanywa na watumishi hao na kuwa sasa wanachokifanya ni kukutana nao na kuelezana ili baadae watapoanza kuchukua hatua kusiwepo na kulaumiana.
Alisema kuwa changamoto ya dawa inayopatikana katika hospitali zetu ni matokeo ya utendaji hafifu kwa baadhi ya watendaji katika idara kwa kuwa serikali ilishatoa muongozo mzuri wa upatikanaji wa dawa na kuwa ukosefu wa dawa katika baadhi ya hospitali ni uwizi na kutowajibika kikamilifu kwa watendaji hao.
‘’sisi kama wizara tumebaini madudu mengi yanayofanywa katika hospitali zetu na ndiyo maana tumekubaliana tupite kwanza kwa watumishi tuwafunde ili ukifika wakati tusilaumiane kutokana na maamuzi hayo magumu’’alisema
Awali mkuu wa wilaya Nkasi Said Mtanda alimweleza naibu waziri kuwa ujenzi wa hospitali ya wilaya umekamilika kwa asilimia 97 kwa maana ya miundo mbinu yote imekamilika na Tshs,Bil.1.8 zimeshatumika kwenye ujenzi wa hospitali hiyo.
Alisema kuwa kilichobaki sasa ni kuanza rasmi kwa kazi katika hospitali hiyo na kuiomba serikali iwapelekee mahitaji muhimu yanayotakiwa ili sasa hospitali hiyo ya wilaya ifunguliwe rasmi na watu kuendelea kupata huduma za kiafya katika hospitali hiyo ya wilaya
Ndipo naibu waziri alipomtaka mganga mkuu wa wilaya aandike mahitaji muhimu yanayotakiwa kwenda MSD haraka ili hospitali hiyo ianze kufanya kazi mara moja
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.