Mkuu wa mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amewataka wataalamu wa lishe kuongeza kasi ya utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa matumizi ya vyakula bora na vyenye virutubisho kwa Watoto wenye umri chini ya miaka 5 ili kufikia malengo ya serikali katika kutokomeza hali ya udumavu na utapiamlo mkali.
Ameyasema hayo baada ya kutembelea banda la Halmashauri ya wilaya ya Kalambo na kusisitiza wataalamu wa afya na lishe kuongeza kasi ya utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya vyakula bora kwa Watoto ikiwemo uanzishaji wa mashamba Darasa ya mboga mboga na matunda.
Aidha kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Rukwa Makongoro Nyerere kupitia ziara ya ukaguzi wa mabanda ya mkoa wa Rukwa ameelezea kufurahishwa na uongozi wa halmashauri ya Kalambo kwa kuanzisha mpango wa utoaji wa unga lishe wa Samaki kwa Watoto chini ya miaka mitano na kusisitiza wananchi katika mikoa ya nyanda za juu kusini kuyatumia maonesho hayo katika kujifunza mbinu mbalimbali za kilimo, ufugaji na uvuvi.
Pamoja na mambo mengine amewataka wataalamu wa lishe kuwafundisha na kuwasimamia wajasiliamali namna nzuri ya usindikaji wa vyakula mbalimbali ili viwe na ubora kwa watumiaji na wanapovitumia waweze kupata virutubishi vya kutosha.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Iringa Kheri James ametumia fursa hiyo kuwataka wajasiriamali na wadau kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi zinatangazwa kikamilifu ili kuongeza wigo wa masoko na kuchochea ushindani wa soko ili kuinua kipato cha wananchi na kutoa ajira kwa vijana.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.