Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ametoa siku sita kwa wakusanya mapato wa halmashauri nne za mkoa huo ambao hawajawasilisha makunsanyo yao benki ili kuweza kusomeka katika mfumo wa kukusanya mapato ngazi ya halmashauri(Local Government Revenue Collection Information System – LGRCIS).
Amesema kuwa wadaiwa hao wanatakiwa kurudisha shilingi 1,217,350,090.85 ya mapato ambapo hadi tarehe 23.9.2019 fedha hizo zinasomeka kwenye mfumo lakini bado hazijapelekwa benki na hivyo kuhisiwa kuwa zimo kwenye mifuko ya wadaiwa hao huku halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ikiongoza kwa kuwa na deni kubwa la shilingi 695,288,837.45.
Ameyasema hayo katika kikao maalum cha kuwasilishiwa taarifa ya hali ya mapato Mkoani humo iliyofanywa na timu ya uhakiki na ufuatiliaji wa mapato ya ndani kwenye mfumo iliyoongozwa na Katibu Tawala msaidizi seksheni ya serikali za Mitaa, kikao ambacho kimehudhuriwa na wakurugenzi, wakaguzi wa ndani pamoja na maafisa TEHAMA wa halmashauri.
“Hawa wadaiwa wote hawa ambao majina yao ninayo hapa, wako wengi, wengi sana, ninawapa siku sita, wadaiwa wote wawe wamerudisha fedha hizi, zote zirudi na siku kama hii wiki ijayo jumanne wote waje hapa, ntakaa nao kikao, wawe wamemaliza madeni yao yote na mifumo yenu yote muwe mmeikamilisha na katika kikao hicho kutakuwa na kamati ya ulinzi na usalama wote tutakuwa hapa, sina mchezo na upande wa kukusanya mapato, tusipokusanya vizuri inamaana hata ile 10% ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu haitatolewa vizuri,” Alisisitiza.
Aidha, Alimuagiza Katibu Tawala wa mkoa kuhakikisha anawalinda wakaguzi wa ndani ambao ndio jicho la kwanza ndani ya halmashauri kabla ya kuingia kwa mkaguzi wa nje na kuwataka wakaguzi hao kutokatishwa tamaa na mtu yeyote mwenye lengo la kujipatia umaarufu wa kisiasa na kuongeza kuwa mapendekezo yanayotolewa na wakaguzi hao ni wajibu kufanyiwa kazi kwa haraka ili kuepukana na hoja za ukaguzi kutoka kwa wakaguzi wa nje.
Awali akitoa taarifa ya uhakiki na ufuatiliaji wa mapato ya ndani kwenye mfumo wa kielektroniki, Katibu Tawala msaidizi seksheni ya Serikali za Mitaa Albinus Mgonya alisema kuwa miongoni mwa masuala yaliyobainika katika ukaguzi huo ilionekana kuwa kuna tatizo kubwa la kuwepo kwa matumizi ya fedha kabla ya kupelekwa benki na mapato mengine kuwepo kwenye mikono ya watu kwa muda mrefu hali ianyopelekea kujikopesha na kushindwa kurudisha.
“Upo udanganyifu kwenye baadhi ya vituo vya kukusanya mapato kama vile stendi za mabasi, Minada, maegesho ya magari n.k ambapo watoa ushuru kwa maana ya wateja hawana uhitaji wa risiti kulingana na uharaka wao kwenye kazi zao, pia kuna udhaifu kwenye usajili wa POS (Point Of Sales Machine) ambapo baadhi ya halmashauri zimebainika kusajili kwa jina la sehemu au cheo mfano VEO au WEO badala ya jina la mhusika na kusababisha mdaiwa halisi kutojulikana na kuwajibishwa kisheria,” Alisema.
Kwa upande wake mkaguzi wa ndani wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Sigridi Mapunda alioroddhesha changamoto kadhaa ikiwemo udhaifu wa utekelezwaji wa hoja anazoziibua katika kazi yake ya ukaguzi, udhaifu katika ofisi ya mweka hazina pamoja na afisa TEHAMA wa halmashauri kushindwa kushughulikia miamala iliyolipwa ili kuweza kufutwa katika mfumo.
“Wale wakusanya mapato, watendaji wa kata huwa hawawashi zile mashine na hivyo hufanya kazi ‘offline’ wanapokuja kuchukua bili huwa wanawasha muda mfupi mara ile miamala inapofunguka wanapewa bili ambayo ni ndogo kwasababu miamala mingine inakuwa bado haijafunguka lakini baadae katika mfumo madeni ya wale wakusanyaji yanapanda kutokana na kufunguka kwa ile mialamala,” Alisema.
Hadi kufikia tarehe 23.9.2019 mapato ambayo hayajawasilishwa (defaulters) kwa Manispaa ya Sumbawanga ni shilingi 45,454,992,68, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ni Shilingi 695,288,837.45, Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo ni Shilingi 255,883,853.32 na Halmashuri ya Wilaya ya Nkasi ni Shilingi 220,722,407.40.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.