Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo ameitaka Kamati ya maafa ya Mkoa kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu kuanzia ngazi ya Kijiji, Mtaa, Kata, Tarafa hadi Mkoa huku akisisitiza mkazo wa kutolewa kwa elimu hiyo uelekezwe kwa vijana ambao wengi wao wanaonekana kutofuatilia taarifa za habari pamoja na elimu mbalimbali zinazotolewa na vyombo vya habari juu ya ugonjwa wa Corona.
Amesema kuwa vijana wa kisasa kuanzia mjini mapaka vijijini wamekuwa wagumu kusikiliza taarifa ya habari kwenye redio wala kuangalia taarifa ya habari kwenye runinga zaidi ya kujiendekeza kusikiliza muziki bila ya kujali na kutaka kujua serikali inasema nini juu ya kujikinga na maradhi hayo ya Corona.
“Akitembea kuna vitu viko masikioni humu anasikiliza muziki tu, nini serikali inasema kuhusu janga hili hajui, lakini mambo haya yanazungumwa sana kwenye redio, yanasemwa sana kwenye televisheni zetu, program ziko nyingi lakini vijana na kundi kubwa wanaonekana hawana muda wa kufuatilia, tuwarudishe hili kundi kubwa, lijenge tabia ya kufuatilia nini kinazungumzwa kwenye redio, kila redio inazungumza, ziko redio za ndani ziko redio zenye sura ya kitaifa,” Alisisitiza.
Aliongeza kuwa hii inaweza kuwa vita ya tatu ya dunia isipokuwa adui hatumuoni hivyo hatuna budi kila mmoja kwa nafasi yake akaendeleza kutoa elimu bila ya kuchoka ili kuweza kupambana na adui huyu ambaye haijulikani lini atashindwa.
Ameyasema hayo wakati alipofanya kikao na kamati ya maafa ya mkoa iliyowajumuisha waganga wakuu wa wilaya wakiongozwa na mganga mkuu wa mkoa, viongozi wa dini na wataalamu wa ustawi wa jamii pamoja na maendeleo ya jamii wa mkoa na taasisi zisizo za kiserikali zinazojihusisha na kutoa elimu za afya katika mkoa.
Aidha, Alisisitiza ili kuweza kufanikisha kufikisha elimu kwa wananchi wote wa mkoa huo hakuna budi kuwaelimisha viongozi wa ngazi zote wakiwemo wenyeviti wote wa vijiji na mitaa ili watilie mkazo utekelezaji wa maelekezo ya serikali katika maeneo yao ya kiutawala.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.