HALMASHAURI ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa imefanikiwa kukusanya shilingi bilioni 3, kufikia jana katika makusanyo ya ndani ya bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020 wakati makisio ilikuwa ni kukusanya jumla ya shilingi bilioni 2.432.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Jacob Mtalitinya aliyasema hayo jana katika hafla fupi ya kukabidhi mikopo kwa waendesha boda boda wa kikundi cha New boda boda Saccos cha mjini Sumbawanga ambapo walikabidhiwa boda boda 35 pamoja na fedha kwa vikundi 14 vya watu wenye ulemavu na mikopo yote ikiwa na thamani ya shilingi milioni 110.6.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa mikopo hiyo ni utekelezaji wa sheria ya kutoa mikopo ambapo asilimia 10 ya makusanyo ya ndani inapaswa kutolewa mikopo kwa makundi maalumu ya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu ambapo hivi sasa imetolewa ikiwa ni robo ya nne ya mwaka wa bajeti 2019/2020.
Alisema kuwa tangu mwaka wa bajeti unaolekea ukingoni ulipoanza halmashauri hiyo imetoa mikopo hiyo isiyo na riba kwa makundi hayo na jumla ya shilingi milioni 235.1 zimekwisha tolewa na jumla ya mtu mmoja mmoja 378 wamekwisha nufaika na mikopo hiyo.
Mtalitinya alisema kuwa hilo limewezekana kutokana na wananchi wa kujua umuhimu wa kulipa kodi na ushuru,fedha hizo zimewezesha mikopo hiyo kutolewa kwa watu wengi na mpaka kufikia mwisho wa mwaka huu halmashauri hiyo itafunga hesabu ikiwa imefanikiwa kukusanya shilingi Bilioni 3.2 zaidi ya asilimia mia moja ya makisio ya makusanyo kwa mwaka huu.
Kabla ya kukabidhi mikopo hiyo mgeni rasmi katika hafla hiyo,mkuu wa mkoa wa Rukwa Joachim Wangabo alisema kuwa pamoja na jitihada nzuri iliyofanyika ya kutoa mikopo hiyo,bado kuna tatizo kubwa kwa wanaopewa mikopo hiyo la kurejesha kwani takwimu zinaonesha kuwa katika mwaka wa fedha wa 2018/2019 ilitolewa mikopo ya shilingi milioni 253.2 na zilirejeshwa shilingi milioni 128.2
Katika mwaka wa fedha 2019/2020 halmsahuri hiyo ilitoa pia mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 124.4 lakini fedha iliyorejeshwa ni shilingi milioni 25.3 sawa na asilimia 20 hivyo kuna kazi kubwa ya kuwabana watu wanaochukua mikopo hiyo warejeshe na watambue kuwa mikopo hiyo siyo zawadi na wale wote ambao ni wasumbufu wachukuliwe hatua za kisheria.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.