Wakulima mkoani Rukwa wamelalamikia kukosekana kwa pembejeo pamoja na bei elekezi katika msimu huu wa kilimo hali inayotia hofu kutopata mavuno makubwa kutokana na wakulima wengi kulima bila kutumia pembejeo na kuiomba Serikali kuweka utaratubu maalumu wa kusambaza pembejeo kabla ya msimu kuanza.
Wakiongea wakati wa uzinduzi wa baadhi ya mashamba katika kijiji cha Kalalasi Wilayani Kalambo yaliozinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joachim Wangabo.
Walisema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kucheleweshewa kwa pembejeo za kilimo na kuwalazimu kutumia pembejeo ambazo si bora.
Walisema serikali haina budi kuweka utaratibu maalumu ambao utawawezesha kupata pembejeo mapema kabla ya msimu kuanza .
‘’Tunaiomba Serikali kuanzisha utaratibu mzuri ambao utatuwezesha kupata pembejeo mapema kwani kila mwaka pembejeo hususani mbolea na mbegu zimekuwa zikiletwa kwa kuchelewa sana.”
Aidha, waliipongeza serikali mkoani humo kwa kuweka utaratibu wa kuwatembelea mashambani na kuwa utaratibu huo utawasaidia kwa kiasi kikubwa kuhamasika na kulima kilimo bora na chenye tija.
Afisa kilimo Mkoani humo Ocran Chengula, alisema pembejeo za kilimo zipo za kutosha na kusema shida ni wakulima wengi kuwa na mazoea ya kununua pembeo pindi msimu wa kilimo unapoanza.
‘’Pembejeo zipo za kutosha, tatizo ni kwamba wakulima wengi wamezoea kununua pembejeo wakati msimu unapoanza ilihali kwenye maduka na maghara ya pembejeo katika misimu yote zinakuwa zipo, hivyo wakulima mjipange mnaweza kununua pembejeo muda na wakati wote badala ya kusubiri kuanza kwa msimu, alisema Chengula.
Awali akikagua mashamba ya wakulima Wilayani Kalambo, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joachim Wangabo, aliwasihi wakulima kulima kilimo chenye tija na ambacho kitawasaidia kujikwamua na hali ya kiuchumi.
Alisema kila mkulima anawajibu wa kuwatumia wataalamu wa kilimo kwenye maeneo husika ikiwa ni pamoja na kutumia mbolea na viuatiulifu kwa lengo la kupata mavuno mengi.
‘’Endapo tukifanya hivyo tutaweza kufikia malengo yetu ya kimkoa ambapo mwaka jana tulikuwa na tani laki nne na tisini na nne na mwaka huu tunataka kufikia tani laki saba za mahindi peke yake, lakini tutaweza kufikia kiwango hicho endapo tutalima kilimo chenye tija.” Alisema Wangabo.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.