Mama Samia ameapishwa katika hafla ndogo iliyofanyika katika Ikulu ya Magogoni na kuhudhuriwa na marais wastaafu wa Tanzania na Zanzibar.
Mara baada ya kuapishwa alipigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride maalumu kwa mara ya kwanza akiwa kama amiri jeshi mkuu wa majeshi ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.
Mama Samia mwenye miaka 61, ndio mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huu nchini Tanzania na wa pili Afrika Mashariki
Mama Samia ameapishwa kushika wadhifa huo kufuatia kifo cha rais John Pombe Magufuli kilichotokea Jumatano, Machi 17, 2021.
Rais Samia atashikilia wadhifa huo kwa kipindi kilichosalia cha muhula wa urais mpaka 2025, kwa mujibu wa katiba ya Tanzania.
Katika hotuba yake ya kwanza baada ya kuapishwa kuwa rais wa awamu ya sita, Rais Samia Suluhu Hassan amesema hakuna kitakachoharibika.
"Amenifundisha mengi na amenilea na kuniandaa vya kutosha, tumepoteza kiongozi shupavu. Alikua chachu ya mabadiliko"Rais Samia amesema.
Rais pia alieleza pia kwa hisia namna ambavyo kuchukua kwake hatamu kumekuwa kugumu kwake.
"Leo nimekula kiapo cha juu sana nikiwa na majonzi tele na kukiwa na simanzi kubwa mtaniwia radhi leo nitaongea kwa uchache sana mengine tutazungumza"
Aidha Rais Samia amewataka watanzania kuzika tofauti zao.
"Huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu na kuwa wamoja kama taifa, kufarijiana kuonyesha upendo, undugu wetu, kudumisha amani yetu, kuenzi utu wetu, uzalendo wetu na utanzania wetu."
''Si wakati wa kutazama yaliyopita lakini ni wakati wa kutazama yaliyo mbele. Huu ni wakati wa kuzika tofauti zetu. Huu si wakati wakutazama mbele kwa mashaka bali kwa matumaini.si wakati wa kunyosheana vidole bali ni wakati wa kushikana mikono," Rais Samia ameeleza.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.