SERIKALI ya Japani imetoa msaada wa vifaa vya upasuaji vyenye thamani ya shilingi milioni 139 katika wilaya za Kalambo na Nkasi mkoani Rukwa ambavyo vitasaidia akinamama wajawazito watakao kuwa wajifungua kwa njia ya upasuaji katika wilaya hizo.
Mashine hizo zimekabidhiwa katika kituo cha afya cha Mwimbi wilayani Kalambo na Balozi wa Japani nchini Tanzania, Takeda katshotoshi ambapo mashine hizo katika tarafa ya Mwimbi zitahudumia wakinamama waliopo katika vijiji 40.
Akikabidhi msaada huo balozi huyo, alisema kuwa mashine hizo zimetolewa msaada na serikali ya Japani kutokana na mahusiano mazuri yaliyopo baina ya nchi mbili ya Japani na Tanzania hivyo anaamini mashine hizo zitakuwa msaada kwa akina mama waliokuwa wanalazimika kusafiri umbali mrefu kwaajili ya kufuata huduma za upasuaji.
Naye Mkuu wa wilaya ya Kalambo Julieth Binyura, alisema kuwa msaada huo umetolewa na serikali ya Japani katika wakati muafaka ambapo hivi sasa serikali ya awamu ya tano imejikita katika kuboresha huduma za afya kwa kujenga majengo na kuweka vifaa tiba.
Alisema kuwa wanawake wanaoishi katika kata tisa, vijiji 40 wapatao 75,000 watakao hitaji huduma za upasuaji wakati wa kujifungua watapata huduma kwa kutumia mashine hizo zilizopo katika kituo cha afya cha Mwimbi.
Mkuu huyo wa wilaya alisema kuwa kabla ya kupatikana kwa mashine hizo baadhi ya wanawake waliokuwa wanahitaji huduma ya dharula ya upasuaji kwaajili ya kujifungua walikuwa wanalazimika kusafiri umbali wa kilometa 140 ili kufikia katika vituo vinavyotoa huduma za upasuaji.
Awali akisoma taarifa fupi kwa viongozi hao, mganga mfawidhi wa kituo cha afya Mwimbi Sospiter Mpuya, alisema kuwa tangu kituo hicho kimepokea mashine hizo mwezi April mwaka huu na kuanza kutoa huduma za upasuaji wanawake 62 wamefanyiwa upasuaji na kufanikiwa kupatikana watoto hai 61.
Alisema kuwa mtoto mmoja alipoteza maisha wakati huduma ikiendelea, lakini bila kuwepo kwa mashine hizo huenda idadi ya vifo vya wakina mama wanaohitaji huduma za upasuaji na watoto wanao zaliwa kwa njia ya upasuaji ingekuwa kubwa zaidi ya hiyo kutokana kukosekana huduma za upasuaji za dharula.
Naye kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kalambo Magreth Kakoya , alisema kuwa Halmashauri hiyo imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni kumi kwaajili ya kuzifanyia matengenezo pindi zitakapo haribika ili kuhakikisha huduma hazo kotokosekana.
Pia aliwasihi wananchi kulipa Kodi hali itakayo iwezesha serikali kuboresha huduma za afya na nyinginezo kusaidia kupunguza changamoto zinazo wakabili.
Mmoja wa wanawake waliokuwepo katika hafla hiyo ya kukabidhi mashine hizo Joyce Sikazwe aliishukuru serikali ya Japani kwa kutambua kuwa wakina mama wa tarafa ya Mwimbi wilaya ya Kalambo kuwa wanahitaji mashine hizo ili waweze kuokoa maisha yao na watoto wao.
Aliwasihi wanawake wajawazito kuwa na tabia ya kuhudhuria kiliniki kitendo kitakacho wasaidia wataalamu wa afya kujua Kama wanahitaji huduma za upasuaji hali ambayo itachangia kuendelea kupunguza vifo vya wakina mama na watoto wilayani humo.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.