WAVUVI wilayani Kalambo mkoani Rukwa,wamepata soko la uhakika la kuuzia samaki baada ya halmashauri hiyo kuwaruhusu kuuza samaki kwa kutumia soko la samaki la kimataifa ililojengwa katika kijiji cha Kasanga mwambao wa ziwa Tanganyika wilayani humo.
Soko hilo la samaki lililopo Kasanga ni moja kati ya masoko mawili ya kimataifa yaliyopo wilayani Kalambo ambapo soko jingine ni soko la mazao lililopo katika mji wa Matai, yaliyojengwa kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2011 kupitia mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA), ujenzi wake ulifadhiliwa kwa asilimia 80 na jumuia ya Ulaya(EU) huku halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga, kabla ya kugawanywa na kuanzishwa kwa halmashauri ya wilaya ya Kalambo, ikichangia asilimia 20 ya ujenzi huo.
Lengo la mradi huo, ni kuwaunganisha wakulima ili wawe na sauti moja katika kushawishi na kutetea maslahi yao kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kisiasa.
Soko la kimataifa la kuuzia samaki liko umbali wa kilomita 73 kutoka mji wa Matai ambao ndio makao makuu ya wilaya likilenga kuwanufaisha watu 35,205 wa ukanda wa ziwa tanganyika na watu 238,000 kutoka maeneo mengine ya Wilaya ya Kalambo sambamba na mikoa ya Mbeya,Iringa, Njombe na Ruvuma pamoja na nchi jirani za Zambia, Kongo D.R.C, Rwanda na Burundi.
Soko hilo ni fursa kwa wavuvi watakao kuwa wanauza samaki na mazao yake yatakayo kuwa yakivuliwa katika ziwa tanganyika na kuuzwa maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi kupitia soko la samaki la Kasanga.
Halmashauri ya wilaya ya Kalambo,imewataka wafanyabiashara wote wa samaki wa ndani na nje ya nchi kufika kwa wingi katika soko la samaki la Kasanga ili wapate samaki kwa wingi na wenye ubora wa kiwango cha kimataifa kwa ajili ya kukuza mitaji yao na maendeleo ya Kalambo na taifa kwa ujumla.
Samaki wanaopatikana kwenye eneo hilo ni samaki aina ya Sangara, Kuhe,Migebuka,Samaki wa mapambo,dagaa wakubwa na aina nyingine nyingi za samaki.
Mmoja wa wavuvi waliopo katika Kijiji cha Kasanga mwambao wa ziwa Tanganyika, Skeva Sinyangwe aliishukuru serikali kupitia halmashauri ya Kalambo kwa kuruhusu soko hilo kuanza kutumika kwani litawaondolea changamoto walizokuwa wakikutana nazo hapo awali ambapo walikuwa wakitegemea kuuza samaki wao kwakutumia masoko yaliyopo nchi jirani.
Tuna mshukuru sana mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hii kwa kutuwezesha kuanza kulitumia soko hili kwani tuna imani sasa kuwa uchumi wa wetu utangezeka ‘’walisema.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.