KATIKA kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Rukwa wanafahamu juu ya namna ya kujikinga na Ugonjwa hatari wa Corona, Mkuu wa Mkoa huo Mh. Joachim Wangabo ameanza kuzunguka katika vijiji vya Bonde la ziwa Rukwa katika Wilaya ya Sumbawanga na kutoa elimu juu ya tahadhari ya ugonjwa huo kwa wananchi wanaoishi katika maeneo hayo ikiwa ni hatua ya kuwataka wananchi hao kuachana na tabia, mila na desturi zitakazochangia kuenea kwa ugonjwa huo.
Anasema kuna watu wanatabia ya kukohoa bila ya kuziba midomo yao na hivyo kuwaasa kuacha tabia hiyo na kueleza kuwa miongoni mwa dalili za ugonjwa huo ni kusikia homa kali sana, mafua makali na kichwa kuuma na hivyo kuwataka wananchi hao endapo watahisi dalili hizo ni vyema kuwahi kituo cha huduma za afya kuangalia afya zao na kuwaomba kuwaripoti wageni wote wanaoingia kutoka nje ya nchi katika maeneo hayo ya vijiji.
Akiongea kupitia kikao kilicho shirikisha viongozi wa dini na watu wengine mkuu wa wilaya ya Kalambo Julieth Binyura, alisema serikali kupitia idara ya afya imeaanza kutoa elimu kuzunguka maeneo yote ya mipakani hususani katika maeneo ya Kipwa, Kasanga, Muze, Kilewani na Samazi na kuwasihi wananchi kuendelea kutoa taarifa za uwepo wa wageni kwenye maeneo yao husika.
Awali Waziri wa afya Ummy Mwalimu alisema kuwa serikali inashirikiana na shirika la afya duniani-WHO na wadau katika kuendelea kutekeleza mikakati ya kukabiliana na ugonjwa huu.
Raia wametakiwa kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa huu kadri wanavyopokea taarifa na elimu za mara kwa mara kwa njia mbalimbali.
Hayo yanajiri huku Barani Afrika kukiwa na jumla ya vifo 16 vilivyoripotiwa : Sita nchini Misri, sita nchini Algeria, wawili Morocco, mmoja Sudan na mmoja wa Burkina Faso.
Afrika walau ni bara lililoathirika kwa kiwango cha chini likilinganishwa na mabara mengine, lakini wataalamu wa afya wanaonya kuwa mifumo duni ya afya ya umma inaweza kuzidiwa uwezo haraka.
Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, ananukuliwa na shirika la habari la AFP akisema , "Afrika inapaswa kuamka... katika nchi nyingine, tumeona jinsi virusi vikiongezeka kwa kasi baada ya kugundulika kwa kisa kimoja.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.