Vifo vya akina mama wajawazito katika Halmashauri ya wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa kwa mwaka 2024 vimepungua kutoka vifo 8 hadi kufikia vifo 5 kwa mwaka 2025 hali iliyochangiwa na ongezeko la vituo vya kutolea huduma za afya ikiwemo Hospitali ya wilaya.
Taarifa kutoka idara ya afya wilayani humo imeeleza kuwa vifo vya Watoto wachanga chini ya mwaka mmoja vimepungua kutoka vifo 38 kwa mwaka 2024 hadi kufikia vifo 9 kwa mwaka 2025 kwa kila vizazi hai 10000.
Aidha vifo vya Watoto wenye umri chini ya miaka 5 vimepungua kutoka vifo 45 kwa mwaka 2024 hadi kufikia vifo 11 kwa mwaka 2025 kwa kila vizazi hai 1000.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Kalambo ndugu Shafi Mpenda kupitia kikao cha Kujadili Sababu za Vifo vya akina Mama Vitokanavyo na Matatizo ya Uzazi na Vifo vya watoto wachanga,Amesema kupungua kwa vifo hivyo kumechangiwa na serikali kuelekeza nguvu kubwa katika kuimarisha huduma za afya ikiwemo ujenzi wa hospitali ya wilaya na vituo vya kutolea huduma za afya.
Hata hivyo Takwimu za Utafiti wa Viashiria vya Huduma za Afya na Malaria (TDHS-MIS) wa mwaka 2022 zinaonesha kuwa kiwango cha vifo vitokanavyo na uzazi nchini ni 104 kwa kila vizazi hai 100,000, wakati kiwango cha vifo vya watoto wachanga ni 38 kwa kila vizazi hai 1,000. Takwimu hizi zinaonesha kwamba bado kuna changamoto kubwa katika kupunguza vifo hivi, hivyo kuna umuhimu wa kuwa na mikakati madhubuti na endelevu ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030 Kwa kupunguza kiwango cha vifo vitokanavyo na uzazi hadi kufikia uwiano wa vifo 70 kwa kila vizazi hai 100,000, na kupunguza vifo vya watoto wachanga hadi kufikia 12 kwa kila vizazi hai 1,000.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.