Wanafunzi wa kike 722 wameshindwa kuendelea na elimu ya msingi na sekondari mkoani Rukwa kutokana na kupata ujauzito wakati shuleni.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Rukwa, Boniface Kasululu, alisema hayo Jana wakati akiwasilisha taarifa ya mpango mkakati wa kudhibiti mimba za utotoni ambao ni matokeo ya kikao cha wadau kilichoitishwa kwa ushirikiano wa Serikali Mashirika ya Plan International, Africare na Jhpiego yanayotekeleza mradi wa uzazi salama mkoani humo.
Alisema kwa mujibu wa takwimu za matukio ya mimba za utotoni katika mkoa huo zinaonyesha kuwa, kwa kipindi cha miaka mitatu (2017/2019) wanafunzi 722 walipata ujauzito.
Alisema kati ya hao, 171walikuwa wa shule za msingi na 551 kwa shule za Sekondari.
Hata hivyo, kwa kuwa Mkoa haukua na makakati madhubuti wa kutafuta na kushughulikia taarifa za mimba za utotoni, ni dhahiri kwamba takwimu hizi ni za chini ukilinganisha na uhalisia.
Mimba za utotoni na uzazi katika umri mdogo ni miongoni mwa changamoto
zinazoukabili mkoa huo, ambapo takwimu za utafiti wa kidemografia za mwaka 2015/2016 zinaonyesha kuwa asilimia 29 ya wanawake wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi19 katika mkoa tayari ni wajawazito au wameshazaa.
Alisema tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa zipo sababu nyingi zinachangia uwepo mimba za utotoni ambapo kati yake ni hali ya umaskini kwa sehemu kubwa ya wananchi, elimu duni, mila, desturi na imani zinazomkandamiza mtoto wa kike.
Malezi hafifu na kuporomoka kwa maadili katika jamii, kutokuwajibika kwa wazazi na viongozi katika ulinzi wa watoto hasa mtoto wa kike, uelewa mdogo wa jamii kuhusu sheria zinazosimamia masuala ya mahusiano ya watoto na wanafunzi.
Pia ukatili wa kijinsia, shinikizo rika, idadi ndogo ya shule za bweni na idadi ndogo ya shule zinazotoa huduma ya chakula cha mchana kwa wanafunzi.
Alisema mkoa una Mikakati kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na shule ya msingi na kila kata inakuwa na sekondari ili kusaidia wanafunzi kutotembea umbali mrefu kwaajili ya kufuata masomo kwa baadhi ya Vijana wa kiume hutumia mwanya huo kuwalaghai watoto wa kike.
Pia kuhakikisha shule za sekondari zinajenga mabweni ya kuishi wanafunzi ambayo yatasaidia wanafunzi wa kike kukaa maeneo ya shule na kupata huduma zote, ikiwepo uangalizi maalumu utakao wahakikishia usalama wao na kupata elimu katika mazingira ya shule bila kutembea umbali mrefu.
Katika mkoa huo Kuna vijiji 59 havina kabisa shule za msingi pamoja na kata 25 hazina sekondari hali inayowalazimu wanafunzi kutembea umbali mrefu kwaajili ya kutafuta elimu na matokeo yake wamekuwa wakiishia kurubuniwa na wanaume kisha kushiriki nao vitendo vya ngono na kupata mimba.
Aidha, Mkuu wa wilaya ya Nkasi, Said Mtanda aliwataka watendaji wa serikali ngazi ya wilaya mkoani kuacha tabia ya kuficha takwimu za mimba hizo kwani kufanya hivyo kutaathiri utekelezaji wa mkakati huo.
Alisema kuwa iwapo watakuwa wawazi katika tatizo hilo,mashirika ya Africare,Plan International pamoja na Jhpiego ambayo yanatekeleza mradi wa uzazi salama mkoani Rukwa yamekuwa pia yakijitahidi kupambana na tatizo la ndoa pamoja na mimba za utotoni,watapata msaada kupitia mashirika hayo ili waweze kutokomeza tatizo hilo.
Mkuu wa mkoa huo, Joachim Wangabo alisema atahakikisha mpango mkakati huo unafika hadi ngazi vijiji na mitaa ili wananchi wauelewe na kushirikiana na serikali katika utekelezaji wake ili malengo kusudiwa yaweze kufikiwa.
Mwisho.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.