Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa imeanzisha utaratibu maalum wa kuwasaidia wananchi kwa kusambaza Madaktari Bingwa katika vituo mbalimbali vya afya lengo ikiwa ni kuondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu kwaajili ya kutafuta matibabu.
Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Aleni Mlekwa alisema kuwa madaktari hao wamesambazwa katika vituo vyote vya afya wilayani humo ambavyo ni kituo cha afya cha Mwimbi, Matai na Ngorotwa.
Alisema kuwa lengo ni kuwezesha wananchi kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kwaajili ya kufuata huduma za matibabu.
Madaktari hao walichukuliwa kutoka hospitali ya mkoa wa Rukwa na wananchi elfu mbili wamekwishatibiwa na zoezi hilo bado linaendelea.
Alisema kutokana na mwitikio wa watu kuwa mzuri wameongea na uongozi wa Wilaya ili katika awamu ijayo bajeti iongozwe kwa lengo la kufikisha huduma hiyo katika zahanati zote za wilaya hiyo.
"Katika zoezi hili tuna madaktari wa aina mbalimbali ikiwemo wa Macho, Madaktari wa magonjwa ya ndani, madaktari wa magonjwa ya akina mama, Madaktari wa magonjwa ya watoto pamoja na Madaktari wa upasuaji na tunaishukuru sana serikali kwa kutoa fedha ili kuwasaidia wananchi wanaoishi katika maeneo ambayo hayafikiki kiurahisi,"Alisema Mlekwa.
Mmoja wa Madaktari bingwa mkoni humo,Hamisi Ulaya alisema mwitikio wa wananchi umekuwa mzuri kwani kila sehemu waliyopita watu walikuwa na uhitaji wa kutibiwa.
Mkuu wa wilaya ya Kalambo Bi. Julieth Binyura, aliwasihi wananchi wilayani humo kuendelea kujitokeza kwa wingi kwenye zoezi hilo ili kupata matibabu katika maeneo hayo.
Alisema lengo la Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha wananchi wanaondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za matibabu na kuwataka wahudumU wa afya kutoa vitambulisho kwa wazee wote.
Baadhi ya wananchi wilayani humo wameipongeza Serikali kwa kusogeza huduma za matibabu karibu na maeneo yao na kuomba kuwa na utaratibu maalumu wa kurudiwa kwa zoezi hilo.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.