BAADA ya mjazito Maria Kalunde(42) na mwanaye Magreth Lui(9) kufa maji wakati wakivuka mto Kalambo akimsindikiza mama yake kwenda Klinik, baadhi ya wanawake wa Kijiji cha Kasitu wilayani Kalambo mkoani Rukwa wameiomba serikali kujenga daraja katika mto huo ili waache kuhatarisha maisha yao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wanawake hao,walisema kuwa wamekuwa wanakabiriwa na changamoto kubwa hasa kipindi cha masika kuvuka mto huo kwakuwa huwa unajaa hadi wakati mwingine maji kupita juu ya kivuko cha miguu kinachokatisha mto huo.
Mmoja wa wanawake hao Isabella Sinyangwe, alisema kuwa katika msimu huo wa mvua nyingi, wanawake wamekuwa wakikabiliwa na wakati mgumu kwakua huduma nyingi ikiwemo za afya zinapatikana ng'ambo baada ya kuvuka mto huo.
Alisema kuwa kuna baadhi ya siku wamekuwa wakiilazimika kukosa huduma hizo kutokana na maji kujaa hadi kupita juu ya daraja hali ambayo ni hatari kwani hawawezi tena kuvuka kwakua hawana uhakika Kama daraja hilo bado lipo au linakuwa limesombwa na maji.
Naye Rozimary Simzosha alisema kuwa hofu pia ipo kwao na watoto wao ambao wamekuwa wakivuka kivuko hicho kwani ni hatari kwakua kimetengenezwa kwa miti na hivyo kuteleza hali inayosababisha baadhi yao kuangukia mtoni na kufa maji.
"Kivuko hicho kimetengenezwa kienyeji sana,na miti ikilowana maji inateleza hivyo ni rahisi hata kwa binaadamu kuteleza na kuangukia ndani ya maji, na kupoteza maisha hivyo tunaiomba serikali ione umuhimu wa kutujengea daraja ili kunusuru maisha yetu" alisema.
Diwani wa kata hiyo Richad Kamagari ,alisema tatizo la vifo kutokana na kutumbukia watu mtoni limekuwa likijitokeza mara nyingi na yeye amekwisha toa taarifa katika baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya ya Kalambo.
Kwaupande wake kaimu katibu tawala wa wilaya ya Kalambo,Mahmood Shauri alisema kuwa serikali itajitahidi kutatua changamoto hiyo inayowakumba wakazi wa kijiji hicho.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.