Wanawake wilayani Kalambo mkoani Rukwa wamesema kuna umuhimu wa serikali kuangalia namna bora ya kudhibiti vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto ambavyo wakati mwingine vimekuwa vikijitokeza katika jamii na kuathiri makuzi na maendeleo ya awali ya watoto hususani wenye umri chini ya miaka 8
Waliyabainisha hayo kupitia maadhimisho ya uzinduzi wa jukwaa la uwezeshwaji kiuchumi la wanawake yaliyofanyika katika kata ya Matai wilayani Kalambo mkoani Rukwa na kusema vitendo vya ukatili wa kijinsia wakati mwingine vimekuwa vikiwaathiri zaidi akina mama wajawazito ambao wamekuwa wakikumbana na ukatili wa aina tofauti ikiwemo vipigo na kusababisha wengine kupoteza viumbe tumboni.
Akiongea kupitia uzinduzi wa jukwaa la uwezeshwaji kiuchumi la wanawake wilayani humo, mwenyekiti wa jukwaa hilo Ester Msigwa, alisema wanawake wajawazito ni miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakikabiliwa na matukio ya ukatili ambao wakati mwingine umekuwa ukiathiri kuhudhuria huduma za afya kama huduma za mama mjamzito.
‘’Pia wanawake wajawazito wameripotiwa kupitia aina tofauti za unyanyasaji ambapo kati asilimia 7 mpaka 10 wametajwa kupitia ukatili wa kijinsia ukiathiri kushindwa kuhudhuria huduma za afya kama huduma ya mama mjamzito, Sambamba na kiwango kikubwa cha ukatili wa kimwili dhidi ya wanawake kimekuwa kikiripotiwa hivyo kuna umuhimu wa serikali Kushirikiana na majukwaa haya ili kusaidia katika utoaji elimu.’’ Alisema Msigwa.
Kaimu afisa maendeleo ya jamii anayeshughulika na makundi ya wanawake,vijana na watu wenye hali ya ulemavu Yasinta Nkyabonaki, alisema kwa kutambua umuhimu wa makundi hayo Halmashauri imetoa fedha kiasi cha shilingi million hamsini ili kusaidia makundi hayo kujikwamua kiuchumi.
Alisema,wanawake wakiwezeshwa watakuwa na uwezo wa kulea familia zao na kuondokana na hali ya ukali ambao wakati mwingine umekuwa ukifanyika pengine kutokana na manyanyaso kutoka kwenye koo au familia zao husika.
Awali akizungumza na hadhara ya wanawake kupitia maadhimisho hayo mkuu wa wilaya hiyo Tano Mwela, alisisitiza wananchi kujiepusha na vitendo vya ukatili kwa kuchukua hatua na kutoa taarifa za uwepo wa matukio hayo kwenye maeneo yao husika ili serikali iweze kuchukua hatua.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.