Waziri wa kilimo, Japhet Hasunga ameagiza kukamatwa kwa kaimu mrajisi wa vyama vya ushirika mkoa wa Rukwa, Anyosisye Mbetwa kwa tuhuma ya kushirikiana mmoja wa mawakala wa pembejeo za kilimo kutapeli vyama vya ushirika zaidi ya Sh milioni 277.
Ametoa maagizo hayo hivi karibuni wakati akizungumza na viongozi wa vyama vya ushirika (AMCOS) mkoa wa Rukwa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa mkoa wa Rukwa mjini Sumbawanga.
Pamoja na mrajisi huyo, pia ameagiza kukamatwa kwa wakala Elias Ndomba mkurugenzi wa kampuni ya Eli Agrovet Co ambao waliahidi kufikishia mbolea kwa wakulima hao kupitia vyama vyao vya ushirika.
Waziri Hasunga alisema kuwa mrajisi huyo ambaye ni afisa ushirika wa mkoa huo, kwa makusudi amekiuka sheria, kanuni na taratibu za vyama vya ushirika hivyo amemshusha cheo hicho na sio afisa ushirika tena.
Alisema afisa ushirika huyo amepoteza sifa ya kuendelea kuwepo katika nafasi hiyo badala ya kuwasaidia wanaushirika yeye anashiriki kuwahujumu.
"Naagiza hawa wote wakamatwe mara moja kwa kuwa wamewatapeli sana ushirika kwa kuchukua fedha zao pasipo kuleta mbolea labda wakileta mbolea hapa ndio waachiwe tofauti na hivyo wafunguliwe mashtaka ya kuhujumu uchumi" alisema Waziri Hasunga.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika cha Ufipa, Anastela Malaji alisema chama kwa niaba ya Amcos 49 kiliingia mkataba na kampuni ya Eli Agrovet ya kusambaziwa mbolea kwa bei elekezi iliyotolewa na serikali amedai kwamba mrajisi aliwataka watoe fedha asilimia 30 ya mbolea waliokuwa wakihitaji.
Alisema makubaliano ilikuwa kampuni hiyo iongeze fedha asilimia 70 kisha kununua mbolea na kuwafikishia wakulima lakini baadae iligundulika haikuwa na mtaji huo, hivyo kuchukua fedha hizo hizo za kwao kununua mbolea kiduchu aina ya Dap na kuwapelekea wakulima hao kinyume na makubaliano yao.
Inasemekana viongozi wa Ufipa walihamisha fedha kutoka katika akaunti yao iliyopo benki ya NMB kiasi cha sh milioni 277 na kupeleka katika akaunti ya Eli Agrovet iliyopo benki ya CRDB ili kusaidia kampuni hiyo kupata mkopo na kuwasambazia wakulima mbolea kwa kadri ya mahitaji yao.
Inaelezwa kuwa makubaliano baina ya chama hicho na kampuni hiyo ilikuwa inunue mbolea ya Dap, Urea na Can na kusambaza kwa wakulima ili waweze kuzalisha mazao yao kwa tija.
Aidha, Katibu wa Mpona Amcos kutoka wilayani Nkasi mkoani Rukwa, Silvester Kapita alisema kuwa kutokana na kuwachangisha wakulima fedha wanalazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuwa wakulima wanahisi viongozi hao ndio wamewatapeli fedha zao.
Alisema Desemba 11 mwaka huu, kampuni hiyo iliwapatia mbolea aina ya Dap lakini kwa wilaya ya Nkasi hivi sasa hitaji lao ni Urea kwa kuwa mahindi tayari yamekuwa marefu na yanaanza kuharibika.
Naye, Mwenyekiti wa Mtema Amcos, Thiofili Kamili alisema wao mahitaji yao yalikuwa tani 555 za mbolea na walichangishana Sh milioni 8 ambayo ni asilimia 30 lakini hawajapata kabisa mbolea hiyo.
Alimuomba Waziri huyo kuona umuhimu wa kuwasaidia kupata mbolea kwa kuwa fedha si hitaji lao kwa sasa.
Aidha, Ndomba alipopewa nafasi ya kuzungumza katika kikao hicho alisema kuwa kuchelewa kwa wakulima kupata mbolea kwa wakati ni kutokana na yeye kutopata fedha kwa wakati katika taasisi za kifedha.
Mwisho.
|
|
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.