Wanateolojia wanatanabaisha kuwa leo ni zaidi ya miaka elfu sita tangu dunia hii iumbwe pamoja na vitu vyote vilivyomo ndani yake akiwemo mwanadamu wa jinsia ya kiume na kike ambaye kwa mjibu wa maandiko, ndiye haswa mtawala wa viumbe vingine vyote duniani. Wanazuoni hao wanakwenda mbali zaidi na kuifananisha dunia na kontena linalosafiri kwa kasi kubwa yaani zaidi ya kilomita elfu saba kwa saa na safari hii ikienda sawia na mabadiliko ya kiikolojia, sayansi na tekinolojia pamoja na mila na desturi kutoka jamii moja kwenda nyingine.
Aidha katika vitabu vitakatifu, mwanamke ametajwa mara chache sana kuliko mwanaume ambapo kwa mjibu wa Biblia takatifu kwenye kitabu cha Mwanzo sura ya 3; 16, mwanaume ni mtawala wa mwanamke.
Mtazamo huu unapingwa vikali na wanaharakati wa kike, wasomi na wenye nguvu kiuchumi wakitetea haki na hadhi sawa kwa wote kama moja ya maazimio ya Protokali ya Beijing ya mwaka 1995, iliyofanyika nchini China na kuibua sintofahamu katika suala zima la malezi na makuzi ya mtoto hasa wa kike katika tamaduni nyingi za familia ya Afrika.
Na hiki ni kimbunga kipya kilichovuma kutoka Ulaya ya mashariki na kulikumba bara la Afrika hata kwetu Tanzania. Awamu hii sasa wanawake wakidai haki sawa kwenye ajira, umiliki na mgawanyo wa mali nyumbani, urithi, elimu, vyeo na kushirikishwa kwenye maamuzi kuanzia ngazi ya familia hadi taifa ambapo katika mkutano huo iliazimiwa kuwa ifikapo mwaka 2030, pawepo na asilimia 50 kwa 50 ya uwakilishi katika vyombo vya kutunga sheria duniani kote na kwamba kila ifikapo machi 8 ya kila mwaka dunia nzima iadhimishe siku ya Mwanamke duniani ikilenga kudai na kulinda haki za mwanamke popote pale alipo.
Kama Falsafa inavyotukumbusha kuwa kila kitu hapa chini ya jua kina chanzo [the philosophical point of causality],harakati hizi zilianza mwaka 1957 ambapo kundi la akinamama waliokuwa wakifanya kazi viwandani Jijini Copen Hagen nchini Denmark, walianza kulalamikia mazingira magumu kazini na kudai haki sawa kuanzia kazini hadi nyumbani kwani walikuwa wakifanyishwa kazi ngumu na kwa saa nyingi sawa na wanaume, wakati wakifika nyumbani wanasubiliwa tena na majukumu ya kifamilia ambayo hayawahusishi wanaume. Hoja yao ya msingi ni kwamba walikuwa wananyonywa mara mbili yaani wakiwa viwandani wananyonywa na mfumo wa Ubepari na wakirudi nyumbani wananyonywa na mfumo dume [Patriachal system].
Nchini Tanzania, mkataba huu wa Beijing ulipokelewa na wanawake wasomi na wale waishio mijini kwa shangwe na ndelemo huku Serikali nayo ikiendelea kutekeleza kipengere kimoja baada ya kingine ambapo mwaka 2020, Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii jinsia na watoto imeagiza kila mkoa kufanya maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani na kauli mbiu ni ‘’Kizazi cha Usawa kwa Maendeleo ya Tanzania ya sasa naya baadaye.’’
Mariam Kimashi yeye ni Bibi Maendeleo na Mratibu wa kitengo cha kuzuia na kupambana na UKIMWI [CHAC] katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo. Alipo kutana na Mwana habari wetu ofisini kwake, alimwambia kuwa hivi sasa haki, wajibu,usawa na hadhi ya mwanamke hapa nchini zinalindwa na kama taifa tumepiga hatua kubwa.
‘’Hivi sasa wanawake wa Tanzania wamejitambua, wametoka utawani na kuanza kujishughulisha na biashara ndogondogo hadi kubwa na wamefanikiwa kutoa mchango chanya kiuchumi kuanzia ngazi ya familia hadi taifa badala ya kubweteka na kuwa tegemea waume zao kwa asilimia zote.
‘’Hata katika Nyanja ya elimu tunashuhudia ongezeko la watoto wa kike kuanzia msingi hadi vyuo vikuu ikilinganishwa na awali ambapo baadhi ya makabila yalikuwa hayaoni umuhimu wa kumpeleka mtoto wa kike shuleni yakimchukulia kuwa ni wa hasara kwani mwisho wa siku ataolewa na kuondoka na kipato chake na kuiacha familia ya wazazi wake bila kitu.’’
Mawazo ya Mariamu yana mashiko ya kitaaluma kwani tangu kusainiwa kwa mkataba huu wa haki sawa kwa wote, tunashuhudia familia nyingi zikiishi maisha bora na upendo hasa zile zenye wazazi waliofikiwa na elimu hii kwa usahihi. Familia itoayo haki sawa kwa watoto ndio msingi imara wa maendeleo ya taifa la Tanzania linalojiandaa kuingia kwenye uchumi wa kati[viwanda] ambao unahitaji wasomi wataalamu waliobobea ili waweze kustahimili ushindani katika soko gumu la ajira.
Tunaona pia vyombo mbalimbali vya uhamasishaji na utoaji elimu juu ya haki za wanawake vikiundwa japo kuwa vinaishia mijini lakini kwa hakika ni mwanzo mzuri kuelekea mafanikio. Vyombo hivyo ni pamoja na TAWLA [Tanzania Women Lawyers Assocition], TAMWA [Tanzania Media Women Association],TGNP [Tanzania Gender Network Progress] na madawati mengine ya jinsia katika vituo vya Polisi na kwenye Halmashauri zote nchini.
Eva Mkunda ni Afisa Mwajiri Mwandamizi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa. Kinacho mfurahisha ni kupungua kwa wateja katika dawati la malalamiko hasa yale yanayohusu unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake.
‘’Jamani hongereni wanaume wa Kalambo na viunga vyake, nawatia shime na kuwaomba muongeze bidii kutekeleza na kutoa elimu ya usawa kijinsia katika jamii na kutokomeza kabisa nyanyasaji wa mwanamke. Upande wetu sisi Waajiri tutaendelea kutoa likizo za uzazi na unyonyeshaji watoto hatutaki utapiamlo hapa.
‘’Mpaka sasa wanawake wa Tanzania wana haki ya kuteuliwa na kugombea nafasi mbali mbali kuanzia vijiji hadi taifa na huu ni ukombozi kwetu.’’ Anaongeza Afisa Mwajiri Eva.
Bila shaka Eva anapata ujasiri wa kusema haya baada ya kuwaona akinamama wakuu wa Wilaya, mikoa, Mawaziri na Wabunge kama vile Mwalimu Julieth Binyura [DC. Kalambo],Dr. Rehema Nchimbi [RC.Singida], Anna Ngwila [RC. Kilimanjaro], Angelina Mabula [Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na maendeleo ya makazi],Ester Ikupa [Naibu Waziri Sera, Bunge, Uratibu na Ulemavu], Injinia Stela Martini Manyanya [Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji],Angela Kairuki [Waziri wa Madini],Profesa Joyce Ndalichako wa Elimu, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama Sumia Suluhu Hassani pamoja na wanawake wengi waliofanikiwa na ambao ni mifano hai inayoonesha kuwa wanawake wanaweza wakithubutu.
Takwimu zinaonesha kuwa idadi kubwa ya watu Tanzania na duniani kwa ujumla hivi sasa ni wanawake na watoto na kwa misingi hiyo, kundi hili halitakiwi kubezwa kwani hata nadharia nyingi za uchumi zinathibitisha kuwa ukiwa na watu wengi ina maanisha una vinywa vingi vya kulisha na kujilisha. Kwa maana nyingine kama nikununua bidhaa na huduma wanawake kwa wingi wao wananunua kwa kiasi kikubwa kuliko wanaume. Hivyo akina mama wanatakiwa wawezeshwe ili wazalishe zaidi kwa ajili ya mstakabali wa uchumi wa nchi na dunia kwa ujumla wake.
Mtaalamu wa mambo ya watu Mwanafalisafa wa Kimarekani profesa Thomas Maltus katika nadharia yake ya ongezeko la watu duniani [The Maltusian theory of Population], anasema watu duniani wanaongezeka kwa mtindo wa kujirudufu progressively wakati uzalishaji wa chakula na huduma za kulilea hili kundi zinaongezeka kwa mtindo wa kupungua yaani arthimetically. Kauli inayoonesha wazi kuwa hali hii isipopatiwa ufumbuzi wa haraka, kuna uwezekano wa kutokea balaa la njaa,vita ya maji na mtikisiko mkubwa wa uchumi kwani watu wanaoongezeka walio wengi ni masikini wa kipato na wanaishi kwa gharama ya chini ya dora moja ya Kimarekeni kwa siku bila kujali wapi waliko.
Naye Padri wa kikatoliki kutoka Jimbo la Moshi na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo kikuu cha Mtakatifu Augustine [Mtwara] Professa Aidani Msafiri,katika kitabu chake kiitwacho ‘’Utandawazi Unaojali’’ [The Globalization of Concern] anapendekeza kuwapo mgawanyo sawa katika matumizi ya rasilimali za dunia kwani matajiri ambao ni kundi dogo sana duniani wanawanyonya walio wengi ambao ni masikini wa kutupwa na kwa misingi hiyo anasema chuki na mapigano yatazidi kuongezeka siku hadi siku duniani kwa kuwa utandawazi uliopo hauwajali walio wengi.
Katika kitabu hicho, Padri Profesa Aidan Msafiri anakuja na nadharia iitwayo The World Economic Shampaign ambapo na yeye anakili wazi kuwa watu walio wengi hivi sasa duniani ni wanawake tena wengi wao wanaishi vijijini na wamegubikwa na wimbi kubwa la umasikini wa kipato.
Anasema asilimia 85 ya utajiri wa dunia unatumiwa na watu asilimia 4na hawa ni matajiri wakubwa wanaomiliki makampuni duniani kote, asilimia 10 ya utajiri wa dunia unatumiwa na watu asilimia 11 na asilimia 85 ya watu duniani wanagombania hiyo asilimia 5 ya rasilimali iliyosalia na kusema kuwa hawa kama ni chai basi hawainywi ila wana ramba nje ya kikombe kilichobeba chai ambao kwa lugha rahisi walio wengi miongoni mwa hawa ni kundi la wanawake ambalo kwa halisi iliyopo ndiyo haswa wahanga wa manyanyaso na kudharauliwa yatokanayo na mfumo dume hasa kwenye nchi za dunia ya tatu.
Hata hivyo, bado jamii haina elimu sahihi juu ya mahitaji muhimu na mchango wa mwanamke katika maendeleo ya nchi kiuchumi ,kisiasa na kiutamaduni. Hii ikiwa ni pamoja na wanawake walio wengi kutojitambua na kuzitambua haki zao ili waweza kuzidai na tatizo hili ni kubwa zaidi hasa kwenye jamii za wakulima na wafugaji waishio vijijini.
Jamii hizi hazitambuwi ni wakati gani mwanamke afanye kazi gani na lini apumzike, chakula gani ale akiwa mjamzito na wakati wa kunyonyesha .Matokeo yake ni kufanyishwa kazi ngumu bila kumpuzika hatimaye kukosa maziwa vifuani kwa ajili ya watoto wachanga na ndipo tatizo la udumavu linapoanzia pamoja na kwamba kuna vyakula vingi nyumbani. Ikitolewa mfano katika mkoa wa Rukwa unaoongoza kwa udumavu wakati ni mmoja kati ya mikoa inayozalisha chakula kwa kiasi kikubwa hapa nchini.
Bado mwanamke anabaguliwa kwenye umiliki wa mali na maamuzi nyumbani na kuchukuliwa kama chombo dhaifu kisicho kuwa na mchango wowote katika makuzi na maendeleo ya jamii. Monica Stanslausi Kabyelo Mhasibu Mwandamizi Katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo anathibitisha haya;
‘’Hata inapotokea kuhoji baadhi ya mambo nyumbani ,mama huambulia kipigo kikali na hatimaye kuendelea kumpeleka mwanamke katika giza nene la utumwa kisaikolojia na tabia hii isiyofaa haiwaachi salama baadhi ya ndugu zetu wa mikoa ya Mwanza,Shinyanga, Simiyu, Geita na Tabora ambao hawajabadili misimamo ya kimila na desturi.’’
Hivyo wakati tunajiandaa kuingia kwenye uchumi wa kati, sisi kama taifa tuungane pamoja kutoa elimu ya jinsia kwenye jamii yote ili itambue nafasi ya mwanamke katika ujenzi wa taifa lenye haki na usawa. Wanawake wajitokeze kwenye kazi za ujenzi wa taifa na waonyeshe uwezo wao kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni. Wanaume waache kuwapiga wake zao kwani ni udhalilishaji ambao hautakiwi kwenye dunia ya leo na ni uvunjaji wa sheria za nchi.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.