Halmashauri ya Kalambo mkoani Rukwa imefikia asilimia 85 ya utekelezaji mpango wa lishe kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa kugawa dawa za vitamini A na minyoo kwa Watoto 61,231 wenye umri kati ya miezi 6 hadi 59 sawa na asilimia 106 ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wazazi na walezi katika shule 102 kuchangia chakula shuleni.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Dkt. Emmanuel Muhanda kupitia kikao cha utekelezaji afua za lishe robo ya nne, amebainisha kuwa katika kuhakikisha Watoto wenye umri chini ya miaka 5 wanaondokana na adha ya utapia mlo na udumavu kwa mwaka wa fedha 2025/2026 halmashauri imetenga fedha kiasi cha shilingi million themanini na tano ambazo zitasaidia kutokomeza hali ya udumavu kwa watoto.
Kwa upande wake Afisa lishe Wilayani humo Robart Tepeli, amebainisha kuwa licha ya hilo katika kufanikisha zoezi hilo halmashauri imefanikiwa kuwafikia wanawake wajawazito na wanaonyonyesha wapatao 1567 katika kata 3 za wilaya hiyo kwa kutoa elimu ya ulishaji Watoto katika siku 1000 za mtoto.
Katibu tawala wilayani humo Servi Ndumbalo kupitia kikao hicho,amesema licha ya hilo halmashauri hiyo imefikia asilimia 73.64 ya utoaji wa chakula kwa wanafunzi shuleni na kuagiza zoezi la utoaji elimu na uanzishaji mashamba Darasa ya kilimo kupewa kipaumbele zaidi.
Licha ya hilo wanufaika 7,434 wa mradi wa TASAF kati yao wanawake wakiwa 7,284 na wanaume 150 wamefikiwa na elimu ya jamii juu ya lishe kwa njia ya vipindi vya radio na mikutano ya hadhara.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.