Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaagiza wakuu wa Wilaya Mkoani humo kusimamia tathmini ya utekelezaji wa mkakati wa miaka mitano (2020 -2025) wa kukabiliana na mimba za utotoni ifikapo mwezi Januari mwaka 2021.
Mh. Wangabo ameagiza kuwa tathmini hiyo ifanyike mwezi Januari 2021 katika ngazi ya Wilaya na Mwezi Februari, 2021 katika ngazi ya Mkoa ili kubaini mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja tangu mkakati huo kuzinduliwa tarehe 18.2.2020
Aidha, alitaja baadhi ya mambo muhimu aliyowasainisha wakuu hao wa wilaya kuwa ni Pamoja na ujenzi wa shule za msingi kwa kila Kijiji, chakula mashuleni, ujenzi wa mabweni ya wasichana katika shule za sekondari na kila kata kuwa na shule yake ya sekondari.
Mh. Wangabo ametoa maagizo hayo wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Kuzuia Ndoa na Mimba za Utotoni Mkoani Rukwa unaotekelezwa na Shirika la Plan International wakishirikiana na mashirika ya PDF, YES TZ, RUSUDEO na RAFIKI SDO huku ukiwa na lengo la kuwawezesha Watoto wa kike kutambua haki zao, kujikinga dhidi ya ndoa za utotoni, kuimarisha mifumo ya ulinzi na haki kwa Watoto Pamoja na kukabiliana na mila potofu.
“Ni matarajio yangu kwamba mradi huu wa kuzuia ndoa na mimba za utotoni mkoani Rukwa, utaleta mabadiliko makubwa kupitia afua na jumbe mbalimbali zilizoandaliwa kupitia elimu ya Afya ya Uzazi na makuzi kwa vijana ya nje na ndani ya shule, ufuatiliaji wa uanzishwaji wa mabaraza ya Watoto, Uwezeshwaji wa miradi midogo midogo kwa wasichana na jamii kiuchumi, mabadiliko ya mila na desturi potofu na uimarishaji wa mifumo ya ulinzi na utetezi wa Watoto katika jamii kwa kipindi chote cha miaka mitano cha utekelezaji wa mradi.”
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Plan International Laurent Wambura alisema kuwa ndoa za utotoni zimeendelea kusababisha madhara kwa Watoto hasa wasichana kwa kukosa nafasi ya kuendelea na elimu, kupata mimba katika umri mdogo, maambukiii ya magonjwa ngono, unyanyasaji wa kijinsia na kingono, vifo visivyotarajiwa wakati wa kujifungua, pia uchumi dhaifu, utegemezi na umasikini
“Ndoa pamoja na mimba za utotoni zimeendelea kuwa ni moja ya changamoto katika kufikia ustawi wa mtoto wa kike hava Tanzania. Katika Tanzania Demographic and HealthSurvey (TDHS) va mwaka 2016, asilimia 36% ya wanawake kati ya miaka 20 hadi 24 waliolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18. Tafiti hii ya TDHS 2016 inaonyesha ongezeko la ndoa za utotoni hasa kwa wasichana kati ya miaka 15 na 19 kwa asilimia 5% kutoka utafiti TDHS wa mwaka 2010,” Alisema.
Halikadhalika, miongoni mwa watu waliohudhuria katika uzinduzi huo alikuwemo Farida Robert ambaye ni mmoja wa wanufaika wa mradi huo ulioanza utekelezaji wake mwezi Januari 2020 na kutegewa kumalika mwezi Disemba 2024, naye alisema.
“Kwa mimi kama mimi nimenufaika san ana huu mradi wa Plan International kwa kuletwa kwentu sisi vijana, maana ni vitu vingi sana vinatokea kwetu vijana kama vile kukosa mahitaji maalum kwa sisi vijana kama vile mavazi na chakula, huu mradi umetunufaisha, umeweza kutuinua kutoka hatua moja hadi nyingine, mimi sasa nashona, napata hela yang una inanisaidia kama msichana na siwezi kutekwa kimapenzi na vijana wa kiume.”
Wakati akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya, Mkuu wa Wilaya ya Nkasi Mh. Said Mtanda alisema kuwa mradi huo katika awamu ya kwanza ulianza na kata tatu katika wilaya ya Nkasi na mafanikio makubwa yalipatikana na hatimae awamu hii ya pili unatekelezwa katika mkoa mzima na hivyo aliliomba shirika la Plan International kuona namna ya kuchukua kata 27 za wilaya hiyo badala ya kata 15.
“Maombi yangu kwa Plan international wakati hawa wengine wanapewa hizi kata sisi tungezimaliza kata zote za wilaya ya Nkasi kama shukrani kwa namna ambavyo tulishiriki katika mradi huu, kwa mfano kata kama Mkinga, Kipili ambazo hazimo katika orodha hii ni maeneo ambayo nilitoa maoni sana kwamba mimba za utotoni na Watoto kuacha shule ni maeneo ambayo yameathirika sana, tulitegemea awamu hii yangepewa kipaumbele, nIna Imani changamoto hii wenzetu mtaishughulikia,” Alisisitiza.
Mh. Wangabo amezindua mradi huo ikiwa ni mwendelezo wa kutekeleza mkakati wa miaka mitano (2020 – 2025) wa kukabiliana na mimba za utotoni Mkoani humo kama alivyoahidi katika salamu zake za kufunga mwaka 2019 kuwa mwaka 2020 utakuwa ni mwaka wa mtoto mkoani Rukwa huku mradi huo ukilenga kuwafikia Watoto 32,167; wasichana wakiwa 22,356 na wavulana 9,811. Pia walezi na wazazi 21,881 katika wilaya 3, Kata 36 na vijiji 116.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.