Mkuu wa wilaya ya Kalambo Mhe. Julieth Binyura amewataka wananchi wenyeji wa wilaya hiyo kuacha wivu dhidi ya wageni kwa kuendelea kuwatuhumu wafugaji wageni kuwa wana mifugo mingi kuliko maeneo waliyonayo. Mkuu wa wilaya ameyasema hayo katika mkutano wa baraza la madiwani la robo ya nne mwaka wa fedha 2017/2018 la halmashauri ya wilaya ya Kalambo uliofanyika tarehe 15 Agosti 2018 katika ukumbi wa chuo cha makateksta katika mji wa Matai.
Mhe. Binyura ameeleza kuwa wenyeji wamekuwa wakiuza maeneo yao kwa wageni, na pindi wageni wanapoleta mifugo yao katika maeneo hayo wanaanza kuwashutumu kuwa na mifugo mingi kitu ambacho wakati mwingine si cha kweli. Mkuu wa wilaya amelieleza baraza hilo kuwa wakati anakuja katika wilaya ya Kalambo alikuta migogoro mingi ya wafugaji kuwa na mifugo mingi kuliko maeneo yao, lakini alitembelea katika maeneo hayo na kutatua migogoro hiyo kwa kuwataka wafugaji wageni kupunguza mifugo yao ili iendane na maeneo yaliyonayo, kitu ambacho wafugaji hao walitekeleza.
Ameeleza kuwa kitendo cha wananchi na waheshimiwa madiwani kuendelea kuwashutumu wafugaji wageni hasa wa jamii wa Kisukuma kuwa na mifugo mingi si kweli na kama ni kweli basi waliwakaribisha wenyewe kwa maana yeye alishatoa zuio la uingizwaji wa mifugo kihorela na bila kuzingatia uwiano wa idadi na maeneo. Pia amewataka wafugaji wenyeji wenye idadi kubwa ya mifugo kuliko maeneo yao nao wapunguze mifugo hiyo na si tu kutaka wafugaji wageni kupunguza mifugo huku wenyeji wakiendelea kuwa na mifugo mingi. Akitoa mfano wa kijiji cha Katapulo, ameeleza kuwa baadhi ya wafugaji wenyeji wa kijiji hicho wana mifugo mingi zaidi ya maeneo yao lakini hawatajwi kama ni wafugaji wenye mifugo mingi kuliko maeneo yao.
Mhe. Binyura amehaidi kuwa, katika kutatua tatizo hilo atawaagiza wataalam kufanya sensa ili kubaini wafugaji wote wenye mifugo mingi kuliko maeneo yao ikiwa ni pamoja na wenyeji ili nao waweze kupunguza mifugo hiyo. Aidha Mhe. Binyura amewataka waheshimiwa madiwani kufanya kazi kikamilifu ya kuwatumikia wananchi katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kudhibiti uingizwaji wa mifugo kiholela ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima baadae. Na kuongeza kuwa serikali ya wilaya ya Kalambo haijashindwa kushughulikia suala la wafugaji.
Mkuu wa wilaya alitoa maelezo hayo wakati akitoa ufafanuzi juu ya suala hilo la wafugaji kufuatia baadhi ya waheshimiwa madiwani kupendekeza ombi la serikali ya mkoa kuja kuwaondoa wafugaji waliohamia kutoka maeneo mbalimbali. Aidha mkuu wa wilaya ameeleza kuwa atakuwa bega kwa bega na waheshimiwa madiwani katika kutekekeza shughuli mbalimbali za kuwatumikia wananchi wa wilaya ya Kalambo.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.