Mwenyekiti wa halmashauli ya wilaya ya Kalambo Mhe. Daudi Sichone amewaonya watendaji wanaohusika katika ukusanyaji wa mapato kupitia mashine za kielektroniki (PoS) kuacha kufanya udanganyifu wa namna yoyote ile pindi wanapotumia machine hizo katika kukusanya mapato ya halmashauri. Mhe. Daudi Sichone ameyasema hayo katika mkutano wa baraza la madiwani la robo ya nne mwaka wa fedha 2017/2018 la halmashauri ya wilaya ya Kalambo uliofanyika tarehe 15 Agosti 2018 katika ukumbi wa chuo cha makateksta katika mji wa Matai.
Mhe. Sichone ameeleza kuwa kuna baadhi ya watendaji ambao huwa wanaomba kufutiwa mihamala ya baadhi ya makusanyo kwa madai kuwa walikosea kukata risiti wakati wa kukusanya mapato ya halmashauri, jambo ambalo linatia shaka na uenda watendaji ambao sio waaminifu wanatumia sababu hiyo. Mhe. Sichone ameeleza hayo wakati akihitimisha uchangiaji wa mbinu ambazo zitumike kuongeza mapato ya halmashauri ya wilaya ya Kalambo katika mwaka wa fedha 2018/2019 mara baada ya uwasilishwaji wa taarifa yenye ufafanuzi juu ya waheshimiwa madiwani kutolipwa posho zao.
Aidha mbinu mbalimbali zilitolewa na baadhi ya waheshimiwa madiwani ili kuboresha mapato ya halmashauri ya wilaya ya Kalambo katika mwaka wa fedha 2018/2019 ikiwa ni pamoja na kuongeza vizuizi na kuongeza nguvu ya ukusanyaji wa mapato katika vyanzo ambavyo havipewi kipaumbele.
Akiongeza katika suala la kudhibiti mapato mkuu wa wilaya ya Kalambo Mhe. Julieth Binyura ameomba kuwasilishwa kwake majina ya watendaji ambao wanahisiwa kufanya udanganyifu katika ukusanyaji wa mapato ya halmashauri ili aweze kutumia vyombo vyake vya ulinzi na usalama katika kuwachunguza.
Katika kuhitimisha, Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kalambo Ndugu. Erick Kayombo amelieleza baraza hilo kuwa yeye pamoja na watalam wake wamejipanga vilivyo katika ukusanyaji wa mapato katika mwaka wa fedha uliopo, 2018/2019 iki kuongeza mapato ya halmashauri.
Aidha kupitia mkutano huo baraza liligeuka na kuwa kamati ya maadili na kumfukuza kazi Afisa kilimo msaidizi daraja la tatu katika kijiji cha Kamawe kata ya Sundu Ndugu. Lusubilo T. Kaswaga kutokana na kosa la utoro.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.