Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo pamoja na timu yake kufika mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa kueleza sababu za kushindwa kutekeleza maagizo saba yaliyoachwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi nchini Mh. Luhaga Mpina juu ya uboreshwaji wa Soko la Samaki la Kasanga ili kuanza kutumika.
Waziri Mpina ambaye aliacha maagizo hayo alipofanya ziara yake ya kikazi katika mkoa tarehe 30.10.2019 na kujionea miundombinu chakavu iliyopo katika soko hilo pamoja na kusikiliza kilio cha wavuvi na wananchi wanaoishi karibu na soko hilo ambalo tangu kuzinduliwa kwake mwaka 2013 na aliyekuwa makamu wa Rais Mh Dkt. Gharib Bilal halijawahi kutumika hadi leo.
Katika kusisitiza hilo Mh. Wangabo alisema kuwa miongoni mwa maagizo yaliyoachwa ni kuwa soko lianze kutumika kuanzia tarehe 31.12.2019 lakini halmashauri haina mpango huo, na kuongeza kuwa soko hilo ni chanzo cha mapato cha halmashauri kwani kukamilika kwake halmashauri itapata ushuru
“Wala msitegemee wizara ndio itafanya kila kitu hapa ili soko liweze kufanya kazi, lazima ninyi mtumie pesa ili mpate pesa, sasa kama hamtumii pesa kuuvuta umeme kutoka pale, ilikuwa ni changamoto kubwa mkasema hakuna transfoma tukamwambia meneja wa TANESCO leta transfoma akaleta ile pale mwaka jana, kutoa pale ule umeme kuja hapa imekuwa shughuli mnataka mwaka mwingine uishe, viongozi waendelee kutoka Dodoma, Dar es Salaam wanakuja hapa kwaajili ya mambo madogo madogo, haiwezekani, amkeni,” Alisisitiza.
Wakati akisoma taarifa ya mkoa juu ya utekelezaji wa maagizo hayo ya waziri Kaimu Katibu Tawala msaidizi seksheni ya Uchumi na Uzalishaji Respich Mayengo alisema kuwa Waziri mpina aliagiza kufanyika kwa maandalizi ya kuhakikisha kwamba soko la samaki linafanya kazi kuanzia tarehe 1.1.2020 na hivyo masuala yote yakamilike ndani ya miezi miwili kutoka 30.10.2019.
“Soko halijaanza kufanya kazi kwa kuwa mfumo wa umeme ndani ya soko haujakamilika licha ya kuwekewa transfoma, elimu na hamasa kwa wavuvi wa kata ya Kasanga na samazi haijatolewa na Katibu Tawala Mkoa alimwandikia DED Kalambo barua kuhusu kuanza kufanya kazi kwa soko hili na kutekeleza maelekezo ya waziri na kumpa ‘deadline’ ya terehe 20.1.2020 lakini hadi sasa barua hiyo haijajibiwa,” alisema.
Kwa upande wake Afisa Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Sadick Senge katibu wa kamati iliyounda na kwa ushirikiano wa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, katibu mkuu Wizara ya Uvuvi pamoja na wavuvi wa Kata ya Kasanga, alisema kuwa hivi karibuni wizara ilituma timu kufanya tathmini ya gharama (BOQ) kwaajili ya miundombinu ambayo wizara inaweza kuichukua
“Baadhi ya miundombinu hiyo ambayo wizara inaweza kuifanyia kazi ni Blast freezer, kuweka mashine na jengo la Soko lakini pia ilikuwa imefanya BOQ kwaajili ya mradi wa barafu na vilevile kuweka mtambo wa utakatishaji maji (water treatment plant) kwaajili ya kuzalisha barafu,” Alisema
Wakati alipopewa nafasi ya kuwasemea wavuvi wa Kata ya Kasanga Mwenyekiti wa Wavuvi hao Khalfan Saidi ameshauri kuwa umeme uwashwe ili mashine ya barafu ifanye kazi na barafu zikiwepo samakai watakuwepo, na kutahadharisha kuwa bila ya kuwepo kwa barafu hizo wavuvi hawawezi kuuza samaki wao kwenye soko hilo.
“Cha ajabu tangu wameweka transfoma pale kuunganisha tu umeme pale kwenye zile jenereta ili umeme uwake mwezi umeisha, kuunganisha tu pale mwezi umeisha kwahiyo imekuwa ni kila siku wakija tunazungumzia hili hili la kusema soko lifanye kazi, wavuvi wako tayari kuleta samaki hapa, sasa unamuamrishaje mvuvi kuleta samaki hapa hata barafu hakuna akileta samaki zake zisipouzikana hawezi kuhifadhi matokeo yake watu hukimbia na samaki zao vijiji, kwasababu vijijini kuna watu wenye friza wanatengeneza barafu,” Alisema.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.