Wanazuoni wa leo [Contemporary Philosophers], wanaunga mkono usemi wa mwenzao Thomas Maltus kwamba uwepo wa watu wengi katika jamii fulani ni uwepo wa vinywa vingi ya kulisha. Tanzania ya leo inayokadiriwa kuwa na watu milioni 60, ni moja kati ya nchi nyingi zilizo kusini mwa jangwa la Sahara yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha nafaka za aina aina zikiwemo mahindi,mtama, maharage na mazao mengine mengi ya mizizi.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na taasisi ya Hifadhi Nafaka Salama [2019] inayofadhiliwa na shirika la DANIDA kutoka Denimark, inaelezwa kuwa Tanzania huzalisha tani milioni 6 za mahindi kila mwaka, lakini asilimia 15 mpaka 40 ya mazao haya hupotea kuanzia kipindi cha mavuno hadi yanapo pelekwa sokoni. Kitendo hiki ni miongoni mwa vipengele vinavyo sababisha upungufu wa chakula hapa nchini ukiachilia mbali kupungua kwa rutuba ardhini, ukame na mafuriko yakiwa ni zao halisi la mabadiliko ya tabia ya nchi kufuatia uharibifu wa mazingira na utandawazi usio jali [The Globalization of un concern].
Wilaya ya Kalambo ni moja kati ya Wilaya tatu mkoani Rukwa zinazo zalisha chakula kwa wingi hasa mahindi, maharage, alizeti na mazao mengine mengi. Wilaya ina eneo la km za mraba 4,715 kati ya hizo 4,211 ni nchi kavu na 504 zimefunikwa na maji ya ziwa Tanganyika kwenye mipaka ya nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Zambia. Kwa mjibu wa Afisa Takwimu wa Wilaya Mjanaheri Swaleh, kuna kaya 54,279 na jumla ya watu 289,345 wakiwemo wanaume 139,970 na wanawake 149,375 ambao wote hawa ili waishi wanahitaji chakula, hewa safi, malazi bora na salama.
Nicholas Mrango ni mkuu wa Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika katika Wilaya ya Kalambo. Yeye anasema uzalishaji wa chakula mwaka huu wa 2019/2020 umepanda ikilinganishwa na mwaka jana. Akitolea mfano wa zao la mahindi peke yake, Mrango anadokeza kuwa uzalishaji umeongezeka kwa asilimia 41 kwa kuzalisha tani 122,926 tofauti na mwaka jana ambapo tani 81,695.5 zilizalishwa. Mafanikio haya yanatokana na uwajibikaji wa pamoja kuanzia ngazi za vijiji mpaka makao makuu ya Wilaya kwani mbolea na pembejeo zingine za kilimo ziliwafikia wakulima kwa wakati na wataalamu wa kilimo waliendelea kutoa elimu kwa kuwafuata wakulima mpaka mashambani, suala lililochangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uzalishaji wa chakula na mazao mengine Wilayani hapa.
‘’Niwasihi wananchi wote kutunza chakula kilichopatikana, ziada inaweza kuuzwa kwa ajili ya mahitaji ya lazima na maendeleo ya familia lakini akiba ya kutosha itunzwe mpaka mavuno yajayo ili kuepukana na adha ya njaa wakati wa masika.’’Ana sisitiza Mrango.
Akiongelea suala la utunzaji salama wa chakula, Afisa Kilimo Mrango anashauri wakulima watunze nafaka kwa kutumia mifuko ya Tarpauline na hermatik isiyo tumia sumu ya kuua wadudu. Anasema nafaka zikitunzwa kwenye mifuko hiyo, hudumu kwa muda usiopungua miaka mitatu bila kubunguliwa na inapatikana kwa bei nafuu hapa hapa mkoani Rukwa. Suala litakalo punguza matumizi ya chakula chenye sumu [ food poison] ambalo limekuwa ni tatizo duniani kote.
Hata hivyo, baadhi ya shughuli za kibinadamu zimekuwa chanzo cha uharibifu wa mazingira na hivyo kusababisha mvua nyingi zisizotarajiwa. Erasto Mwasomola ni Mtaalamu mwandamizi wa misitu katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo. Yeye anazitaja baadhi ya shughuli hizo kuwa ni pamoja na ukataji miti usiokuwa endelevu, uchomaji moto na upimaji viwanja usio zingatia utunzaji mazingira yaani kubadilisha mapori kuwa makazi.
Shughuli zingine ni kupanuka kwa kilimo cha Mpunga ambacho pamoja na mambo mengine, huzalisha gesi ya Methane amabayo huathiri anga la juu. Kuongezeka kwa viwanda duniani ambavyo katika hali ya kawaida huongeza joto na kuharibu pia anga la juu [Horizone] na hatimaye kubadili kabisa tabia ya nchi, suala ambalo huathiri vibaya uzalishaji chakula duniani.
Mtaalamu Mwasomola anawasisitiza wana Kalambo kufanya uvunaji endelevu wa misitu, kuacha kusafisha mashamba kwa kuchoma moto ikiwa pamoja na kupanda miti ili kuyatunza mazingira.
‘’Kwa kila tunacho kifanya kwa ajili ya maendeleo yetu, tufikirie Zaidi namna ya kuhifadhi mazingira ili nasi yaendelee kutuhifadhi.’’ Anaongeza Erasto.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.