Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wananchi mkoani humo kuhakikisha wanafika katika mabanda ya kutolea elimu ya sheria ili kuitumia fursa ya kupata elimu hiyo inayotolewa bure kwa kipindi cha wiki nzima ya sheria.
Mh. Wangabo amesema kuwa elimu hiyo inayotolewa na Mahakama Pamoja na wadau wengine ikiwemo Mawakili wa Kujitegemea, Serikali, Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mkurugenzi wa uendeshaji wa Mashataka (DPP), Ofisi ya Wakili (Solicitor General), Baraza la Ardhi Pamoja na Taasisi mbalimbali itawawezesha wananchi hao kuona njia za kutatua migogoro mbalimbali.
Amesema kuwa wananchi wamekuwa na malalamiko na migogoro mingi inayohusu mambo ya kisheria na hawajui sheria na hivyo kuwataka kuitumia wiki hiyo ya sheria iliyoanza tarehe 23.1.2021 kupata ushauri katika changamoto mbalimbali za kisheria wanazokabiliana nazo katika kutafuta haki zao.
“Elimu ni ya Bure itumieni hapa, kwa wale ambao watashindwa kufika hapa, wasikilize vyombo vya Habari, wasome magazeti, wafuatilie kule, kuna elimu ya bure ambayo inatolewa wiki nzima hii, tusikilize redio, watumishi wa mahakama wamejipanga, mahakimu majaji wanatoa elimu kule ya bure na wakati mwingine kutakuwa na mawasiliano ya moja kwa moja, unauliza swali lako utajibiwa.”
“Naona watu wengi sana wanamsumbua Mkuu wa Wilaya wakifikiri yeye ndio hakimu yeye ndio Jaji, yeye ndio mwanasheria, mtu anadhani akienda kule migogoro yake yote inaishia kule, sikilizeni fuatilieni vyombo vya Habari, ili muweze kujua masuala ya kisheria, si kila jambo linatatuliwa na mkuu wa Wilaya, Mkuu wa mkoa, Sisi tunafanya upatanishi ili watu waridhiane tu basi, lakini ukitaka haki ni mahakamani,” Alimalizia.
Mh. Wangabo ameyasema hayo wakati akifungua wiki ya sheria nchini leo tarehe 24.1.2021 kwa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, wiki ambayo imeambatana na matukio ya kutembea umbali wa kilomita 9 pamoja na maadhimisho ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Mahakama Kuu nchini.
Aidha, Mh. Wangabo ametumia nafasi hiyo kuipongeza Mahaka kuu ya Tanzania kwa kuadhimisha miaka 100 (karne moja) tangu kuanzishwa kwake mwaka 1921 huku akiwashauri kutafakari kwa kina mambo yanayotakiwa kuboreshwa ili kuendelea kudumisha Amani, Uhuru, Udugu na Haki kwaajili ya ustawi wa nchi yetu.
Wiki hii ya Sheria inaongozwa na kauli mbiu ya miaka 100 ya Mahakama kuu nchini isemayo; “Mchango wa Mahakama katika nchi inayozingatia Uhuru, Haki, Udugu, Amani na Ustawi wa Wananchi 1921 – 2021”.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.