BAADHI wajumbe wa kikao cha kujadili mikakati itakayo tumika kutokomeza mimba za utotoni kwa wanafunzi mkoani Rukwa wamewalaumu baadhi ya wazazi mkoani humo kuwa chanzo kikubwa cha watoto wao kujiingiza katika vitendo vya mapenzi na kujikuta wakipata ujauzito kutokana na kutowapa mahitaji muhimu na hivyo kupelekea kukwamisha ndoto za maisha yao.
Baadhi ya wajumbe wamebainisha hayo mwishoni mwa wiki wakati wakichangia katika kikao cha siku moja kilichoandaliwa na tasisi isiyo ya kiserikali ya Vijana pambana kujiletea maendeleo Rukwa(VIPAMARU) kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Moravian Conference uliopo mjini Sumbawanga.
Mmoja wa wajumbe hao, Israel Mwaisaka, alisema kuwa changamoto kubwa inayowakuta watoto wanaopata ujauzito wengi wao imebainika kuwa wazazi wao wamewatelekeza kwa kutowapa mahitaji ya muhimu kama chakula, mavazi pamoja na malazi mazuri.
Alisema kuwa kutokana na kukosa huduma hizo baadhi ya watoto hao wanalazimika kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi na watu wazima na hivyo kujikuta wakipata ujauzito huku baadhi yao wakiwa ni wanafunzi na hivyo kupoteza ndoto zao za baadaye.
Naye Anna Malisa mjumbe wa kikao hicho, alisema kuwa baadhi ya akina mama hawatimizi wajibu wao katika malezi na kuwaacha watoto wakizurula bila uangalizi hali inayosababisha baadhi ya Vijana wakiume hasa waendesha bajaji na bodaboda kutumia mwanya huo kwa kuwalaghai watoto wa kike na kuanza nao mahusiano ya kimapenzi.
Kwaupande wake Afisa maendeleo ya jamii mkoa wa Rukwa, Dionisia Njuyui, alisema kuwa tatizo jingine lililopo ni watoto hao wa kike kupenda sana kufanya ngono, baadhi yao wamekuwa hawasikii mafundisho ya wazazi na hivyo kujiingiza katika mapenzi na kuishia kupata ujauzito angali wakiwa wadogo.
Alisema kuwa pamoja na changamoto hiyo lakini bado serikali haikati tamaa ndio maana inaruhusu mijadala ya wazi ili kubaini njia ya kukabiliana na tatizo hilo sambamba na kuruhusu kuanzishwa kwa tasisi zinazotoa elimu kuhusu kukabiliana na changamoto hiyo.
Awali mkurugenzi wa tasisi ya VIPAMARU, Anania Mhalila alisema kuwa taasisi hiyo imeamua kujikita kubaini sababu zinazopelekea kuongezeka kwa mimba za utotoni mkoani Rukwa ikiwa ni pamoja na changamoto zinazowakabili watoto wenye umri kuanzia miaka 0-8 na hivyo kutokuwa na makuzi mazuri.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.