KalamboMkuu wa wilaya ya Kalambo Julieth Binyura amemwagiza Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Msongela Palela kuharakisha ujenzi wa kituo cha afya Samazi ili kuwawezesha akina mama wajawazito waishio maeneo hayo, wazee, pamoja na watoto kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu wakati wa kusaka huduma za matibabu katika kituo cha afya Ngorotwa na Matai .
Akiongea baada ya kutembelea maendeleo ya ujenzi wa kituo cha afya Samazi, mkuu wa Wilaya hiyo Julieth Binyura, amesema utekelezaji wa ujenzi wa kituo hicho ni muhimu na umekuja kwa wakati muafaka kwani kata za Kisumba na Samazi hazina vituo vya afya na kwamba wananchi waishio katika maeneo hayo, wanapata adha kubwa kufuata huduma za afya mbali hasa baada ya kupewa rufaa.
Kituo cha afya Samazi kilianza kujengwa mwezi may 2019 baada ya serikali kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 400 ambazo zingetakiwa kujenga majengo matano kwa muda wa miezi mitatu na kukamilika, jambo ambalo halikuwezekana kufuatia mwamko mdogo wa wananchi kujitolea nguvu kazi na hivyo kupunguza idadi ya majengo na kuwa manne ambapo hivi sasa jumla ya majengo matatu pekee yako usawa wa lenta huku ujenzi ukiendelea kwa kasi kubwa.
Wakiongea kwa nyakati tofauti, wananchi waishio katika maeneo hayo, wamesema ni muhimu kituo hicho kika kamilika mapema kwani akina mama wajawazito, wazee na watoto wanasumbuka sana na wakati mwingine kupoteza maisha njiani wakifuata matibabu ya hali ya juu baada ya kushindikana kwenye ngazi ya zahanati za Kipanga, Samazi na Kafukoka.
“kukamilika kwa kituo hiki kutasaidia kuokoa maisha ya watoto wadogo wenye umri kuanzia sifuri kwani akina mama wengi wamekuwa wakisumbuka sana pindi wanapo pata rufaa ya kwenda kujifungua katika kituo cha afya Ngorotwa na Matai ambavyo vyote viko umbali wa Zaidi ya km 38 hadi 78.’’ Walisema wananchi hao.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.