Mkuu wa wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa Dkt Lazaro Komba amewaagiza viongozi wa serikali za vijiji kuwachukulia hatua kali za kisheria ikiwemo kuwafikisha kwenye vyombo vya dola wazazi na walezi wanao kwamisha masomo ya watoto kwa kuwaozesha na kuwapeleka kwenye shughuli za kuchunga mifugo.
Ameyasema hayo kupitia maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika ambayo kwa ngazi ya mkoa yamefanyika katika kijiji cha Msanzi wilayani humo na kusisitiza wanajamii wenye taarifa au ushahidi kuhusiana na watoto ambao haki zao zimekiukwa na wazazi au walezi kutoa taarifa kwenye vyombo vya dola ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yao.
Licha ya hilo alizitaka serikali za mitaa kushirikiana na jeshi la polisi katika kuwatafuta wazazi ,walezi au ndugu wa watoto wanao watelekeza watoto na kusisitiza jamii kuwa sehemu ya kuwalinda watoto kwa kuwazuia kushiriki kwenye michezo ambayo inaweza kusababisha vitendo viovu kufanyika ikiwemo kwenye vibanda vya kuonyesha sinema.
Aidha alizitaka taasisi na jamii kuitikia wito wa serikali katika swala la ujenzi wa mabweni katika shule za sekondari ili kusaidia ulinzi kwa watoto na kwamba hatua hiyo itasaidia watoto kutimiza ndoto zao na kufikia malengo yao.
Baadhi ya walimu mkoani humo wametumia fursa hiyo kuishauri serikali kuona uwezekano wa kuwekeza kwa watoto wenye uhitaji maalumu kwa kuongeza vifaa vya kufundishia na kujifunzia hatua itakayo saidia kuongeza ufaulu na kufikia malengo yao ya baadaye.
Maadhimisho ya siku ya mtoto wa afrika hufanyika kila ifikapo Juni 16 ya kila mwaka huku yakiwa na lengo la kukumbuka mauaji ya watoto 176 ambao waliuwawa wakati wakidai haki za kutobaguliwa pamoja na kupata elimu bora na kupinga mifumo ya elimu ya kibaguzi iliyoku wepo wakati huo chini ya utawala wa ubaguzi wa rangi wa kikaburu.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.