Wavuvi katika mwambao wa ziwa Tanganyika mkoani Rukwa wameshauriwa kujenga mazoea ya kujiunga kwenye vikundi ambavyo vitasadia kupata mikopo kiurahisi kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.
Ziwa Tanganyika kupitia eneo la Kasanga, Muzi,Samazi na visiwa vyake lina wavuvi wapatao elfu moja na vyombo vya uvuvi mia saba, lakini wavuvi hao wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya soko la kuuzia samaki na hivyo kulazimika kupeleka samaki zao nchi jirani ya Zambia na kuikosesha Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo mapato yatokanayo na mazao ya uvuvi kufuatia kuto tumika ipasavyo soko hilo tangu kujengwa kwake.
Mapema hapo jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Msongela Palela alitembelea na kukagua eneo la soko hilo na kuwaruhusu wavuvi pamoja na wafanyabiashara kuanza kulitumia soko hilo baada kulifanyia ukarabati, kununua na kuweka vichanja pamoja na miundo mbinu ya umeme.
Licha ya hilo, Msongela aliwasisitiza wavuvi kujiunga kwenye vikundi ili iwe rahisi kupata mikopo isiyokuwa na riba kutoka Halmashauri na ambayo itawasaidia kujikwamua kutoka hali duni kiuchumi na kukuza biashara zao.
Kwa upande wake Mweka hazina wa Halmashauri hiyo Agustino Manda, aliwasisitiza wavuvi hao kuendelea kulitumia soko hilo kwa tija, kwani hivi sasa soko limekarabatiwa na kinacho subiriwa ni wavuvi kupeleka na kuuza samaki zao.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.