Wajumbe wa kamati ya lishe endelevu Wilayani kalambo mkoani Rukwa wameazimia kuwachukulia hatua kali za kisheria wafanyabiashara ambao wamekuwa wakiuza chumvi isiyokuwa na madini joto baada ya kuelezwa kuwa inasababisha ugonjwa wa Goita na utapia mlo kwa watoto wenye umri chini ya miaka 5 na kuzitaka mamlaka husika kutekeleza agizo hilo.
Wajumbe hao kwa kauli moja kupitia kikao cha robo ya pili 2019-2020 kilichofanyika katika ukumbi wa mkuu wa Wilaya hiyo, wamesema kumekuwa na changamoto ya baadhi ya wafanya biashara kuuza chumvi isiyokuwa na viwango na hivyo kusababisha hofu kwa walaji.
‘’Tuzitake mamlaka zote zinazohusika kuhakikisha chumvi yote inayouzwa hususani kwenye maduka na kwenye minada inakuwa na madini joto pamoja na kuhakikisha inafungwa kwenye paketi zenye nembo ya shirika la viwango Tanzania TBS.’’ Walisema wajumbe hao.
Akifafanua kikaoni, Afisa lishe wa Halmashauri Doris Lunyungu amesema mbali na kusababisha magonjwa ya goita na utapia mlo, chumvi isiyokuwa na madini joto pia ni chanzo cha kuharibu mimba kwa akina mama, kuzaa watoto wenye matatizo ya akili na mgongo wazi. Akasema azimio hili limekuja kwa wakati muafaka ambapo Wilaya ya Kalambo inakabiriwa na tatizo la ukondefu kwa asilimia 15 na udumavu wa asilimia 0.2 kwa watoto chini ya miaka 5, na kwamba wazazi na walezi watahakikisha wanawapa watoto wao vyakula bora na vyenye virutubisho.
Afisa afya Wilayani humo Richard Manuma, amesema idara ya afya imeanza kutoa elimu kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kudhibiti uingiaji holela wa chumvi isiyo kuwa na viwango.
Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Julieth Binyura akamwagiza Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo kuhakikisha anatekeleza maazimio yote yaliyotolewa na wajumbe wa kamati hiyo. Akasema chakula kilicho patikana kutokana na mavuno ya shamba kihifadhiwe na kiliwe kwa wakati muafaka ili kuondokana na tatizo la utapia mlo na kusisitiza kuzingatiwa maelekezo ya wataalamu wa afya kuhusu kudhibiti kuenea ugonjwa wa Corona ili Wilaya ya Kalambo iendelee kuwa salama.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.