BARAZA la madiwani Halmashauri ya wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa limemuagiza mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo pamoja na jeshi la polisi kuwasaka na kuwakamata waganga wafawidhi wa zahanati ya kijiji cha Kantalemwa pamoja na zahanati ya Kijiji cha Ilango kwa tuhuma za wizi wa mali ya umma.
Agizo hilo lilitolewa mwishoni mwa wiki na baraza hilo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa diwani wa kata ya Kilesha,Benard Maskini pamoja na diwani wa kata ya Mnamba, Jimson Chilulumo.
Katika kikao hicho diwani Maskini wa kata ya Kilesha alilalamikia kitendo cha mganga mfawidhi wa zahanati ya kijiji cha Ilango, Denis Mapori kuwalaghai wajumbe wa kamati ya ujenzi wa nyumba ya kuishi mganga wa zahanati hiyo na kukubali kusaini muhtasari,kisha yeye kwenda benki na kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 24 na kukimbia nazo kusiko julikana.
Alisema kuwa nyumba hiyo iliyojengwa kufikia kwenye lenta, imesimama ujenzi wake tangu mwaka 2010 na baada ya mganga aliyekuwepo alikimbia na fedha za ujenzi ambazo alizitoa benki kwa madai kuwa anakwenda kumlipa mkandarasi ili amalizie ujenzi wa nyumba hiyo.
Diwani huyo alisema kuwa kutokana na zahanati hiyo kukosa mganga kwakua aliyekuwepo alikimbia na fedha,wananchi wamekosa huduma kwa muda mrefu kijijini hapo hali inayo walazimu kutembea umbali mrefu kufuata huduma katika vijiji vingine.
Naye diwani Chilulumo wa kata ya Mnamba alilalamikia katika baraza hilo kitendo cha mganga mfawidhi wa zahanati ya Kantalemwa, Faraja Sanga kuchukua sola iliyokuwa inatumika katika zahanati hiyo na kwenda kuifunga katika kilabu chake cha pombe ili wateja wapate mwanga pindi wanapokunywa pombe.
Alisema kuwa sola hiyo yenye thamani ya shilingi 140,000 ,ilipatikana kutokaana
baada ya wananchi wa kijiji hicho kuchangishana fedha na kuinunua ili isaidie kupata mwanga katika zahanati yao pindi wahudumu wa afya wanapotoa huduma nyakati za usiku lakini mganga wa zahanati hiyo aliamua kuchukua na kuipeleka kwenye kilabu chake cha pombe.
Kutokana na hali hiyo wananchi wa kijiji hicho hasa wakina mama wajawazito wamekuwa wakikabiliwa na wakati mgumu pindi wanapokwenda kujifungua nyakati za usiku kutokana na kukosekana mwanga katika zahanati hiyo.
Baada ya malalamiko hayo ndipo baraza hilo la madiwani kupitia mwenyekiti wake Daud Sichone lilimuagiza mkurugenzi wa Halmashauri hiyo pamoja na jeshi la polisi kuwasaka watumishi hao wa idara ya afya na wafikishwe katika vyombo vya sheria ili wakajibu tuhuma zinazo wakabili.
Hata hivyo mwenyekiti Sichone aliwaonya watumishi wa umma katika Halmashauri hiyo kuacha tabia ya kuhujumu mali za serikali kwani kufanya hivyo Kuna wasababishia usumbufu kwa wananchi na kurudisha nyuma jitihada zao pamoja na za serikali za kutatua changamoto zinazo wakabili.
Kwaupande wake kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo Magreth Kakoyo alikiri kuwepo kwa tuhuma hizo na kuahidi kutekeleza maagizo ya baraza hilo haraka iwezekanavyo ili wananchi waweze kupata haki yao ya huduma bora zinazotolewa na serikali.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.