Nchini Tanzania waumini wa madhehebu mbalimbali wamekamilisha siku tatu za maombi maalumu ya kumshukuru Mungu baada ya 'kupungua' kwa maambukizi ya covid19.
Hatua hii ni baada ya kauli ya rais wa Tanzania John Magufuli ya kuwataka raia wa nchi hiyo kwa imani zao tofauti kwa muda wa siku tatu, kuanzia Ijumaa mpaka Jumapili kumshukuru Mungu kwa kuliepusha taifa na janga la Corona.
Kilele cha maombi hayo pia kimeangukia siku ya Eidul Fitri ambapo waumini wa dini ya kiislamu kutoka maeneo mbalimbali nchini humo wamejitokeza kwa ajili ya swala ya Eid.
Eidul Fitr inafuatia kukamilika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan ambapo waislamu hufunga kwa muda wa mwezi mmoja.
Katika msikiti mkuu wa Gaddafi uliopo jijini Dodoma ujumbe mkuu uliotawala kwa mamia ya waumini, wake kwa waume waliojitokeza ni ule wa kuchukua tahadhari ya corona.
Waziri Mkuu wa Tanzania Kaasim Majaaliwa alikuwa ni mmoja wa waumini walioswali Eid katika msikiti huo wa Gaddafi, ambao ni miongoni mwa misikiti mikubwa na maarufu zaidi nchini.
Akizungumza na waumini jijini humo baada ya swala, Waziri Mkuu alitoa takwimu mpya za waliopona lakini aliendelea kusisitiza kuhusu kuchukua tahadhari.
"Tunaendelee kuwa na tahadhari ili kupunguza uwezekano wa maambukizi, suala la kunawa mikono ni muhimu sana, na unapokuwa katika msongamo vaa barakoa," amesema waziri mkuu.
Tofauti na eid nyingine ambazo waumini wa dini ya kiislamu huonesha upendo wao kwa kupeana mikono, kukumbatiana na hata kutembeleana majumbani.
Mwaka huu, kutokana na janga la corona hali imekuwa tofauti.
"Msikitini baada ya swala kupeana mikono, lakini mwaka huu hakuna. Hata kama ni vitu vya kuongeza upendo lakini tumeshindwa kuvifanya," anasema Maulid Seif mkazi wa Dodoma.
Sherehe za Eid mwaka huu imeenda sambamba na kilele cha siku tatu za maombi maalumu ya kumshukuru Mungu kama alivyoshauri Rais wa Tanzania John Magufuli baada ya kusema maambukizi yamepungua.
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.