Wazazi na walezi wilayani Kalambo mkoani Rukwa wameshauriwa kutoruhusu ndugu na jamaa wanao omba hifadhi kwa muda kulala na Watoto wao majumbani ili kuwaepusha na vitendo vya ubakaji na ulawiti ambavyo wakati mwingine vimekuwa vikijitokeza na kuwasababishia madhara watoto.
Hayo yamebainishwa na mkuu wa dawati la jinsia na Watoto wilayani humo kupitia jeshi la polisi Lucy Mushi wakati akiongea na wananchi kupitia kampeni ya msaada wa kisheria ya Mama Samia katika vijiji vya Kata ya Matai na kusisitiza jamii kuwalinda Watoto wao dhidi ya vitendo vya ukatili ikiwemo vipigo.
Aidha aliwataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wao katika malezi bora kwa kudhibiti Watoto wao kutokwenda kwenye vibanda umiza ili kuangalia video na badala yake wajikite zaidi katika kuwalinda Watoto wao ikiwemo kuwahimiza kujisomea masomo ya darasani.
Kwa upande wake mwanasheria wa serikali kutoka wizara ya Katiba na sheria Doreen Mhina ametumia fursa hiyo kuwataka walimu kuwa sehemu ya kutokomeza ukatili kwa kutoa elimu kwa wazazi na walezi juu ya madhara ya vitendo vya ukatili katika jamii ikiwa ni pamoja na kukaa meza moja na wanafunzi ili kusikiliza changamoto zao.
Hata hivyo baadhi ya wananchi katika maeneo hayo wameiomba serikali kuipitia upya na kuifanyia marekebisho sheria ya ndoa ya mwaka 1971 kwa kuruhusu wanandoa kutengana kwa muda badala ya kutoa talaka ya moja kwa moja ili kupunguza ongezeko la watoto wa mitaani almaarufu kama (chokoraa).
Matai, Kalambo, Rukwa
Anuani ya posta: P.o box 03
Simu ya Mezani: 025-2955212
Simu ya mkononi: +255 622 858 482
Email: ded@kalambodc.go.tz
Copyright ©2018 Kalambo DC . All rights reserved.